Habari za Punde

Kesi 39 za Udhalilishaji zaibuliwa na Mtandao wa Kupinga Udhalilishaji Pemba kwa miezi 5.

 

Mratibu wa TAMWA Zanzibar ofisi ya Pemba, Fat-hiya Mussa Said akizungumza wakati wa mkutano wa Wanantandao wa kupambana na udhalilishaji wa Kisiwani Pemba, uliowashirikisha Wanaharakati. 
Bi.Siti Faki Ali Mwenyekiti wa Mtandao wa kupinga vita udhalilishaji Wilaya ya Wete, mkoa wa Kaskazini Pemba akiwasilisha ripoti ya utekelezaji wa majukumu ya mtandao huo.
Mratibu wa TAMWA Zanzibar ofisi ya Pemba, Fat-hiya Mussa Said akizungumza wakati wa mkutano huo.

JUMLA ya kesi 39 za udhalilishaji wa kijinsia katika Wilaya za Mkoani na Wete Pemba zimeibuliwa na mtandao wa kupinga udhalilishaji wa wilaya hizo katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi mei mwaka huu.

Wakiwasilisha ripoti ya ufuatiliaji wa matukio hayo katika jamii kwa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ)  wanamtandao hao wameeleza kuwepo kwa mitandao ya kupinga udhalilishaji katika jamii kumesaidia kuongeza hamasa kwa wanajamii kuwa tayari kujitokeza kuripoti taarifa za matukio ya kesi za udhalilishaji wa kijinsia jambo ambalo limechochea uchukuaji wa hatua dhidi ya matukio hayo katika ngazi mbalimbali.

Mwenyekiti wa mtandao huo Wilaya ya Mkoani, Haji Shoka alisema katika utekelezaji wa majukumu ya mtandao huo wamefanikiwa kufuatilia kesi kumi kwenye wilaya hiyo ambazo zipo katika hatua mbalimbali.

“Kuanzia mwezi Januari hadi Mei kwa wilaya ya Mkoani tumeibua kesi kumi za udhalilishaji ambapo kati ya kesi hizo, kesi nne zipo kwenye vituo vya polisi zikiendelea na upelelezi, kesi nne zipo mahakamani na kesi moja mtuhumiwa katoroka na nyingine moja imesuluhishwa nyumbani,” alieleza mwenyekiti huyo.

Aidha alieleza kutokana juhudi za mitandao hiyo kufanya mikutano ya uelimishaji jamii kwenye jamii juu ya kupambana na vitendo hivyo, hatua hiyo imesaidia kubadili mitazamo ya wanajamii kupunguza usuluhishi wa kesi hizo majumbani.

Alifahamisha, katika kutekeleza kazi zetu, mtandao umefanikiwa sana katika mambo mawili, kwanza jamii nyingi zimeanza kubadilika na wanaripoti matukio ya kesi za udhalilishaji katika sehemu husika tofauti na zamani ambapo walikuwa wanaripotiu kwa sheha na kupelekea kesi nyingi kusuluhishwa katika ngazi ya familia jambo ambalo lilipelekea wahanga wa matukio haya kuathirika zaidi kisaikolojia.”

Aidha alibainisha kuwa katika kipindi hicho mtandao ulifanya mikutano ya utoaji elimu ya udhalilishaji kwa watoto kupitia skuli na madrasa ikiwa na lengo la kuwatayarisha watoto kutambua viashiria vya udhalilishaji na namna ya kujikinga navyo.

Alisema, “kwa mwaka huu pia tuliendelea na zoezi la utoaji wa elimu katika maeneo mbalimbali ambapo tumetembelea madrasa na skuli mbalimbali na jumla ya watu 1,374 kati yao wanawake 748, na wanaume 626 tumewafikia.”

Nae Siti Faki Ali, mwenyekiti wa mtandao huo Wilaya ya Wete alisema kwa upande wa wilaya hiyo walifuatilia na kuibua kesi 29 ambapo kati ya hizo kesi za ubakaji zilikuwa 14.

“Katika wilaya ya Wete tumefanikiwa kufuatilia na kuibua jumla ya kesi 29, kesi za ubakaji zikiwa ni kesi 14, kutorosha sita, shambulio la aibu nne, kunajisi mvulana nne, kumpa mimba mwari kesi moja ambapo kati ya hizo, kesi 20 zinaendelea na upelelezim na hakuna kesi iliyotolewa hukumu kwa kipindi hiki,” Siti Faki ali, mwanamtandao,” alieleza.

Akizungumzia kuhusu utoaji wa elimu ya udhalilishaji mwenyekiti huyo alibainisha kwamba Jumla ya watu 2,115 walifikiwa na elimu hiyo kati yao wanawake wakiwa ni 1,270 na wanaume 845.

Mapema mratibu wa TAMWA Zanzibar ofisi ya Pemba, Fat-hiya Mussa Said aliwataka wanamitandao hiyo kuendelea kufikisha elimu kwenye jamii ili kuisaidia kuwa na taaluma ya kutosha ya kujilinda dhidi ya matukio hayo.

“Wanamtandao tuna jukumu kubwa sana la kusaidia wananchi kujua namna ya kutafuta na kupata haki zao hasa matukio haya ya udhalilishaji, na huu ni wajibu wetu kwa pamoja kuhakikisha tunawalinda wanawake na watoto dhidi ya matukio yote ya udhalilishaji katika jamii,” alisema Fat-hiya.

Mkutano huo wa uwasilishaji ripoti ya utekelezaji wa majukumu ya mtandao wa kupinga udhalilishaji Pemba ni sehemu ya utekelezaji mradi wa kutumia jukwaa la Habari kumaliza vitendi vya udhalilishaji wa Kijinsia unaotekelezwa na TAMWA ZNZ kwa kushirikiana na Shirika la kimataifa la maendeleo la Denmark (DANIDA).

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.