Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein
Ali Mwinyi amepongeza juhudi zinazochukuliwa na uongozi wa Eneo Huru la
Biashara Barani Afrika (AfCFTA), katika kuhakikisha nchi wanachama
zinashirikiana ipasavyo.
Rais Dk.
Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Katibu
Mtendaji wa Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA), Bwana
Wamkele Mene.
Katika
mazungumzo hayo, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa ana matumaini makubwa kwamba
juhudi hizo zinazochukuliwa kwa makusudi zitasaidia kwa kiasi kikubwa kufikia
lengo lililokusudiwa na nchi wanachama wa Eneo Huru la Biashara Barani Afrika
(AfCFTA) katika kuimarisha uchumi na kuleta maendeleo endelevu.
Rais Dk.
Mwinyi alieleza jinsi alivyofurahishwa kwa kupata taarifa kwamba Eneo Huru la
Biashara Barani Afrika (AfCFTA), imetoa mazingatio maalum kwa nchi za visiwa
ikiwemo Zanzibar.
Alisema kuwa
amefurahishwa na mafanikio yanayoendelea kupatikana katika Mkataba wa Eneo Huru
la Biashara Barani Afrika (AfCFTA), ambapo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni
mwanachama.
Aidha, alisema
kwamba atahakikisha Zanzibar inashirikiana na nchi wanachama wa Eneo Huru la
Biashara Barani Afrika (AfCFTA) katika mipango yake ya kuimarisha Sera ya
uchumi wa buluu ambayo ndio dira ya uchumi wa Zanzibar hivi sasa na tayari
imepewa kipaumbele na nchi wanachama wa Mkataba huo.
Rais Dk.
Mwinyi alimuhakikishia Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara
Barani Afrika (AfCFTA), Wamkele Mene kwamba Serikali zote mbili ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zitahakikisha
wafanyabiashara na wawekezaji pamoja na wananchi wote kwa jumla wanatumia fursa
za masoko na uwekezaji zilizoko katika Mkataba huo.
Sambamba na
hayo, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa atahakikisha wafanyabiashara na
wajasiriamali waliopo nchini wanapewa elimu ya kutosha ili kuweza kutumia fursa
zilizoko katika soko la nchi wanachama wa (AfCFTA).
Nae Katibu
Mtendaji wa Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA), Bwana
Wamkele Mene alimueleza Rais Dk. Mwinyi jinsi alivyofarijika kupata fursa ya
kuja Zanzibar kwa mara ya pili.
Katika maelezo
yake, Katibu Mtendaji huyo alieleza miongoni mwa malengo ya ujio wake ni pamoja
na kuja kutoa elimu ya uwelewa na malengo ya Mkataba wa (AfCFTA) kwa Kamati ya
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Baraza la Wawakilishi la
Zanzibar ambapo mafunzo hayo yanatarajiwa kufanyika siku ya Jumaapili ya Mei
22, 2022 hapa Zanzibar katika Hoteli ya Sea Cliff.
Aidha,
kiongozi huyo alieleza kwamba uelewa pamoja na malengo hayo yatasaidia kwa
kiasi kikubwa katika kuwawezesha wananchi kufahamu vyema mipango na malengo ya
Mikataba ya Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA), kwa nchi wanachama
wake.
Katibu
Mtendaji huyo wa Sekretarieti ya (AfCFTA), aliipongeza Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwa juhudi zinazoendelea kuchukuliwa katika kuimarisha utekelezaji wa
Mikataba iliyopo tangu kujiunga kwake.
Alitumia fursa
hiyo kueleza jinsi fursa zilizopo kwa nchi ndogo ndogo zikiwemo za visiwa
ambazo zitafaidika moja kwa moja katika mikataba hiyo ikiwemo Zanzibar ambayo
tayari imeshaonesha mikakati yake katika kuimarisha sera ya uchumi wa buluu.
Sambamba na
hayo, kiongozi huyo alitumia fursa hiyo kumueleza Rais Dk. Mwinyi shughuli na
mikakati iliyowekwa na Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA), kwa nchi
wanachama wake pamoja na mafanikio yaliyokwisha patikana.
Imetayarishwa na Idara ya Mawasiliano,
Ikulu Zanzibar. OF
RESPONSIBILITY
No comments:
Post a Comment