Habari za Punde

Mwalusamba atetea nafasi ya Uenyekiti

 

Mwenyekiti wa Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI), Daniel Mwalusamba akila kiapo baada ya kuchaguliwa tena na Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa shirikisho hilo kwa kura 70 kati ya 100 uliofanyika jana kwenye ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Mount Uluguru, mkoani Morogoro.

Na Mwandishi Wetu, Morogoro.                                                                                                 

WAJUMBE 70 kati ya 100 wa mkutano mkuu wa uchaguzi wamemchagua Daniel Mwalusamba kuwa Mwenyekiti wa Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI), katika uchaguzi uliofanyika jana kwenye ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Mount Uluguru, mkoa wa Morogoro.

Msimamizi wa uchaguzi huo uliosimamiwa kwa umahiri mkubwa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Leonard Thadeo alisema nafasi hiyo iliwaniwa na wanamichezo wawili, ambapo Eliud Mwaiteleke alipata kura 30; huku nafasi ya Makamu Mwenyekiti ikichukuliwa na Alquine Masubo aliyepata kura 64 na kuwashinda Kaundime Kizaba mwenye kura 18 na Chilemba Chikawe kura16.

Thadeo alisema Alex Temba amechaguliwa kwa kura 80 kuwa Katibu Mkuu na kumshinda Mussa James mwenye kura 20; na Katibu Msaidizi alichaguliwa Mariam Kihange aliyepata kura 56 na kuwashinda Mfaume Mfaume (21), Andrew Sekimweri (14) na Mwinjuma Bwanga (7); na huku Rose Makange aliyekuwa hana mshindani ameshinda kwa kishindo nafasi ya Uweka Hazina Mkuu kwa kuzoa kura zote 100.

Wajumbe wawili wa Viti Maalum wanawake wameshinda Itika Mwankenja kwa kura 81 na Bahati Mollel kwa kura 68, huku Assumpta Mwilanga alishindwa kwa kupata kura 37; na wajumbe watano wa Kamati ya Utendaji walioshinda ni Tumsifu Mwasamale (91), William Moye (89), Apolinary Kayungi (85), Damian Manembe (83) na  Mashaka Mwamage (74), huku Fidelis Choka (57) alishindwa.

Hatahivyo, Thadeo amesema wanamicbezo 21 ndio waliojitokeza kuwania nafasi mbalimbali, huku wapiga kura walikuwa 100, ambapo amewashukuru wagombea wote kwa kushiriki vyema hatua zote ikiwemo ya awali ya usaili na baadaye uchaguzi bila ya kuwa na matatizo, hali kadhalika kwa wapiga kura nao kufuata taratibu na kanuni zilizokuwa zimewekwa na BMT na kufanikisha uchaguzi huo salama.

“Wanamichezo wameitikia wito na kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali tangu ilivyotangazwa hata kwenye usaili walioweza kufika ni 16 baada ya watano kushindwa kufika na ndio waliochujwa, na kimsingi uchaguzi ulikwenda vizuri sana maana tulipata ushirikiano mkubwa kutoka kwa wenzetu na pia hatujapata malalamiko kutoka kwa wagombea walioshindwa,” amesema Thadeo.

Naye Mwalusamba aliwashukuru wajumbe kwa kumchagua tena katika nafasi ya Uenyekiti kwa kuwa wameonesha imani kubwa katika utendaji wake wa kazi na kumpa dhamana ya miaka minne tena ya kuongoza, ambapo ameahidi kwa kushirikiana na viongozi wenzake wa kamati ya utendaji watahakikisha wanatekeleza maazimio yote waliyojiwekea kwenye mkutano mkuu.

Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI), wakifuatilia kwa makini masuala yaliyokuwa yakielezwa na msimamizi wa uchaguzi huo, Leonard Thadei (hayupo pichani) kwenye ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Mount Uluguru,, mkoani Morogoro.
Msimamizi wa uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI), Leonard Thadeo (aliyenyoosha kidole) wakati akizungumza na wajumbe waliokasimiwa madaraka na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kusimamia uchaguzi huo wakiwa wanazungumza mambo mbalimbali baada ya zoezi hilo kukamilika jana kwenye ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Mounti Uluguru, mkoani Morogoro.  
Mmoja wa wajumbe wa uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI), Mohamed Ally (wapili kulia) akisimamia zoezi la kuhesabu kura za wagombea wa nafasi ya ujumbe wa kamati ya utendaji katika uchaguzi uliofanyika jana kwenye ukumbi wa Hoteli ya Mount Uluguru, mkoani Morogoro.
Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI), wakifurahia jambo wakati wa mchakato wa upigaji kura uliofanyika jana kwenye ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Mount Uluguru,, mkoani Morogoro.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.