Habari za Punde

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan Awasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar Akitokea Nchini Oman Baada ya Kumaliza Ziara Yake.

 

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Viongozi wa Serikali alipowasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar, akitokea Nchini Oman baada ya kumaliza ziara yake ya Siku Tatu Nchini humo, (kulia kwa Rais) Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Philip Isdor Mpango, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi, Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Mhe. Idrisa Mustafa Kitwana na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama Tanzania alipowasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar, akitokea Nchini Oman baada ya kumaliza ziara yake ya Siku Tatu Nchini humo.,


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Wazee wa Baraza la Wazee wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar alipowasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar, akitokea Nchini Oman baada ya kumaliza ziara yake ya Siku Tatu Nchini humo.,

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameungana na viongozi mbali mbali wa Kitaifa katika mapokezi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akitokea nchini Oman.

Mapokezi hayo yamefanyika Alaasiri ya leo huko katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Kisauni Zanzibar ambapo viongozi kadhaa walihudhuria katika mapokezi hayo akiwemo Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Philip Mpango.

Wengine ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa, Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Injinia Zena Ahmed Said, Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama, viongozi wa vyama vya siasa, dini pamoja na viongozi wengine wa Serikali.

Rais Samia aliwasilini kiwanjani hapo akiwa pamoja na viongozi kadhaa aliofuatana nao katika ziara yake hiyo kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ndege ya Serikali akitokea nchini Oman ambapo kiongozi huyo alifanya ziara hiyo ya siku tatu ya Kiserikali.

Akiwa nchini Oman, Rais Samia alipata fursa ya kufanya mazungumzo na viongozi mbali mbali akiwemo mwenyeji wake kiongozi Mkuu wa Taifa la Oman Sultan Haitham bin Tariq Al Said, pia alishiriki kongamano la wafanyabiashara wa Oman na  Tanzania na kushuhudia utiaji saini makubaliano ya ushirikiano wa pamoja katika sekta mbali mbali.

Aidha, alifanya mazungumzo na Mufti Mkuu wa Oman Sheikh Ahmed bin Hamad Al-Khalili pia, alifanya mazungumzo na viongozi wanawake wakiwemo wakuu wa Taasisi mbali mbali za nchini Oman pamoja na kutembelea kituo cha Saratani cha Dar Al Hanan kilichopo Mjini Muscat nchini Oman.

Sambamba na hayo, Rais Samia alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara wa Oman kuja kuekeza Tanzania na kuwaeleza fursa mbali mbali zilizopo nchini ikiwa ni pamoja na mazingira mazuri na nguvu kazi ya kutosha.

Imetayarishwa na Idara ya Mawasiliano,

Ikulu Zanzibar. F RESPONSIBILITY

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.