Habari za Punde

Uzinduzi wa Maadhimisho ya Miaka 25 ya Taasisi ya Mama Anna Mkapa.

 

SERIKALI zote mbili zitaendelea kuandaa mazingira rafiki na kufanya kazi kwa karibu na wadau wote katika kuimarisha ustawi wa wananchi na ujenzi wa  nchi.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi alisema hayo wakati wa halfa ya uzinduzi wa sherehe za maadhimisho ya miaka 25 ya Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote (EOTF), Jijini Dar es Salaam.

Dk Mwinyi alisema hayo yanafanyika kwa kuwa jukumu la serikali zote ni kuandaa mazingira yatakayowezesha sekta binafsi na asasi za kiraia kushiriki katika kufanikisha utekelezaji wa mipango ya maendeleo.

Alisema program za kuwezesha wanawake wajasiriamali, elimu na afya za EOTF ni muhimu kwa maendeleo ya nchi.

“Ile ya kupambana na umaskini kwa makundi mbalimbali ya wanawake ina umuhimu wa pekee, ikizingatiwa kwamba kuna changamoto nyingi za kiuchumi na kijamii zinazoyakumba makundi mbalimbli ya wanawake ambao ndio idadi kubwa ya nguvu kazi kwa taifa letu,” alisema.

Kwa mujibu wa Rais Mwinyi, juhudi za kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kuwapatia mitaji, elimu na kuwatafutia masoko ya bidhaa zao ni muhimu katika kuondoa changamoto ya ajira inayoathiri kundi kubwa la wanawake na vijana hivi sasa.

“Ni ukweli usio na shaka kwamba serikali zetu haziwezi kuajiri vijana wote wanaomaliza masomo yao katika ngazi mbalimbali. Ni lazima tuwape njia na mbinu mbadala za kujiajiri kama inavyofanywa na mfuko huu.

“Vile vile program nyingine mbili mnazoziendesha katika sekta ya afya na elimu nazo zina umuhimu mkubwa, tukizingatia kwamba, ili tuweze kujenga taifa bora, ni lazima tuwe na nguvu kazi yenye afya na elimu inayoendana na wakati na mahitaji tuliyonayo,” alisema

Dk Mwinyi alisema EOTF ni mdau muhimu wa serikali  katika kuimarisha ustawi wa watoto, vijana na wazee wa jinsia zote.

“Kama tujuavyo serikali ina majukumu mengi na mzigo mkubwa wa kutekeleza mipango yake ya maendeleo na utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Kwa hiyo misaada inayotolewa na asasi zisizo za kiserikali za kitaifa, kikanda na kimataifa pamoja ile inayotolewa na washirika wa maendeleo ni muhimu ili kuweza kufikia malengo yetu,” alisema.

Alisema mfuko huo ni mfano bora wa ushirikiano na serikali unaopaswa kuigwa na asasi nyingine za kiraia za ndani nan je ya nchi.

Awali Mwenyekiti wa mfuko huo Anna Mkapa alisema kwa miaka 25 wamekuwa mstari wa mbele katika nyanja ya kuondoa umaskini kwa wanawake kwa kuwawezesha wajasiriamali 6,000 kutoka Bara na Visiwani kupata mafunzo ya ujasiriamali,

Pia kutangaza na kuuza bidhaa zao kupitia maonyesho mbalimbali na kujipatia zaidi y ash trilioni 11, ikiwa ni pamoja na kuzalisha ajira zaidi ya 25,000.

program nyingine aliyoitaja ni kusaidia kwenye elimu kwani imetoa ufadhili kwa watoto 1755 kutoka kwenye familia duni kupata elimu kutoka chekechea, shule za msingi, sekondari, Veta hadi vyuo vikuu vya ndani na nje.

Alieleza Program nyingine ni ya afya ambayo imesaidia mama na mtoto kwa kujenga hospitali, zahanati, vituo vya afya, magari ya kubebea wagonjwa, vifaa vya hospitali, viti mwendo kwa hospitali, shuleni na watu binafsi.

Alisema pia katika kutatua tatizo la watoto yatima na wa mitaani katika jamii, wamejenga kituo cha watoto yatima Mtaa wa Simbani Kibaha.

Akielezea changamoto alieleza kuwa ni ukosefu wa fedha za kutekeleza huduma kwa jamii, vifaa vya kutendea kazi na mahali pa kufanyia kazi wanapojiandaa kuendeleza huduma za uanzishwaji wa program ya ‘Women Busines Centre’

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.