Habari za Punde

DIPLOMASIA KUENDELEA KUWA CHACHU YA KUKUZA NA KUBIDHAISHA KISWAHILI DUNIANI


Kushoto Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda na Waziri wa Elimu wa Afrika Kusini, Mhe. Matsie Angelina Motshekga wakitia saini makubaliano ya kuanza kufundisha kiswahili katika elimu ya msingi nchini Afrika Kusini.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango ametoa rai kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuweka jitihada za makusudi za kukikuza Kiswahili nje ya mipaka ya Tanzania.

Rai hiyo imetolewa wakati wa sherehe za maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani yaliyofanyika kitaifa Leo tarehe 7 Julai 2022 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Mhe. Mpango akiwa Mgeni Rasmi katika maadhimisho hayo ameeleza kuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeendelea kubeba jukumu la kizalendo ambapo, kupitia Balozi zake ilifanikiwa kushawishi majukwaa ya kimataifa kuitambua lugha ya Kiswahili na kupewa siku ya kuadhimishwa duniani ambayo inafanyika leo kwa mara ya kwanza.

“Ninatoa pongezi kwa Balozi zetu kwa jitihada wanazofanya za kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili, nimeona mitandaoni jinsi Balozi zilivyojitoa kufanya makongamano na midahalo ya Kiswahili katika kusherehesha siku hii” alisema Mhe. Mpango.

Pamoja na kutolewa kwa pongezi kwa Wizara, Mhe. Mpango ametoa pongezi za kipekee kwa Mabalozi wa Tanzania wanaowakilisha Jijini New York, Marekani, Mhe. Kennedy Gaston; Addis Ababa, Ethiopia, Mhe. Innocent Shio na Paris, Ufaransa, Mhe. Samuel Shelukindo kwa kukamilisha mchakato wa kutambulika kwa Kiswahili duniani.

Aidha, uwepo wa siku maalum ya kuadhimishwa lugha ya Kiswahili duniani kukupa nguvu ikiwa ni lugha rasmi ya kazi katika Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na kufanya jumuiya nyingine ambazo Tanzania ni mwanachana kuipa upekee lugha ya Kiswahili.

Naye Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia na Mwakilishi wa kudumu katika Umoja wa Afrika, Mhe. Balozi Innocent Shio ameeleza kuwa lugha ya Kiswahili ina nafasi kubwa katika kukuza na kuimarisha mtangamano kwa maendeleo ya Afrika kwakuwa, mawasiliano huleta amani na kuongeza mshikamano.

Pia, akaeleza wakati huu ambapo Umoja wa Afrika unaenda kutathmini Agenda 2030 na kutekeleza kikamilifu Agenda 2063 ya Umoja huo ni wakati sasa wa kukibidhaisha kiswahili ili kuunganisha mataifa ya Afrika na kuweza kuyafikia malengo ya mpango wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCTA) katika kukuza sekta za kiuchumi na kuinua pato la Wananchi na Taifa kwa ujumla.

“Lugha ni bidhaa hivyo ni muhimu kusimamia kikamilifu soko lake ili kuleta fursa zinazotarajiwa, mathalan ajira kwa Walimu, Wakarimali, huduma ya kutafsiri, utangazaji, uandishi wa vitabu vya Kiswahili, Sanaa ya uigizaji na uhariri” alisema Balozi Shio.

Tarehe 23 Novemba 2021, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) lilitangaza Siku Maalumu ya Kiswahili Duniani inayoadhimishwa tarehe 7 Julai kila mwaka.

Sherehe za maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani, zimeandaliwa na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na kuhudhuriwa na Viongozi wa Wizara, Taasisi, Idara, sekta binafsi na taasisi ya za elimu nchini na Wananchi.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango akihutubia wakati wa sherehe za maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani yaliyofanyika kitaifa leo tarehe 7 Julai 2022 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Elimu wa Afrika Kusini, Mhe. Matsie Angelina Motshekga akihutubia wakati wa sherehe za maadhimisho ya Siku ya Siku ya Kiswahili Duniani yaliyofanyika tarehe 7 Julai 2022 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Mhe. Motshekga ameeleza kuwa Serikali ya Afrika Kusini ipo tayari kuingiza somo la lugha ya kiswahili katika shule za msingi na hivyo itaendelea kuhitaji usaidizi wa vitabu na maboresho ya mitaala kwa ajili ya kufundishia.

Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia na Mwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Afrika, Mhe. Innocent Shio akihutubia kwenye sherehe za maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani yaliyofanyika kitaifa leo tarehe 7 Julai 2022 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Fatma Rajab (aliyeshika bendera) akifuatilia sherehe za maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani yaliyofanyika kitaifa leo tarehe 7 Julai 2022 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Kushoto ni aliyekuwa Balozi wa Tanzania na Mwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Mataifa, Balozi Modest Mero na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Bi Ellen Maduhu wakifuatilia sherehe za maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani yaliyofanyika kitaifa leo tarehe 7 Julai 2022 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Kushoto Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda na Waziri wa Elimu wa Afrika Kusini, Mhe. Matsie Angelina Motshekga wakitia saini makubaliano ya kuanza kufundisha kiswahili katika elimu ya msingi nchini Afrika Kusini.

Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Philip Mpango akimshukuru Naibu Waziri wa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mabarouk Nassor Mbarouk baada ya kumlizika kwa sherehe za maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani yaliyofanyika kitaifa leo tarehe 7 Julai 2022 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia na Mwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Afrika, Mhe. Innocent Shio akipokea tuzo ya ngao kutoka kwa Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo, Mhe. Mphamed Mchengerwa kwenye sherehe za maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani yaliyofanyika kitaifa leo tarehe 7 Julai 2022 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Hafla ikiendelea.


Viongozi wa meza kuu wakiwa wamesimama wakati wimbo wa Taifa na wa Afrika Mashariki ukipigwa kwenye sherehe za maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani yaliyofanyika kitaifa leo tarehe 7 Julai 2022 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Naibu Waziri Wizara  ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk.

Picha ya pamoja meza kuuna viongozi Wakuu wa Wizara, Taasisi na Idara za Serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM) 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.