Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali
Mwinyi amesema kuwa taasisi ya Benjamin Wiliam Mkapa licha ya shughuli zake
ambazo zinahitaji nyenzo ili kuyafikia malengo yaliyowekwa bado inahitaji
kupata michango kutoka kwa taasisi na watu mbalimbali kwa ajili ya kuyafikia
malengo hayo.
Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo katika ukumbi wa hoteli ya Madinat Al Bahri, Mbweni Zanzibar wakati wa chakula pamoja na harambee ya kuchangia Mfuko wa taasisi ya Benjamin Wiliam Mkapa.
Rais Dk. Mwinyi alieleza imani yake kwamba wapo wengi walio na imani ya kuichangia taasisi hiyo ili ifikie malengo na matarajio yake.
Aliwashukuru washiriki wa shughuli hiyo kwa ushiriki na moyo walio nao katika kuhakikisha zinapatikana fedha kuiwezesha taasisi hiyo ili iweze kutekeleza malengo yake.
Rais Dk. Mwinyi ambaye pia ni Msarifu Mpya wa Taasisi ya Benjamin Wiliam Mkapa, alieleza jinsi taasisi hiyo inavyofanya kazi kubwa na nzuri kusaidia sekta ya afya katika pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wageni wote waliotoka nje ya Zanzibar kuvitembelea vivutio mbalimbali vya utalii viliopo ili wawe mabalozi wa kuitangaza Zanzibar nje ya nchi.
Rais Dk. Mwinyi alitoa shukurani za dhati kwa niaba ya watendaji wa taasisi hiyo kwa kuitikia wito wa kuja kushiriki pamoja katika kufanikisha Kongamano la siku mbili Zanzibar.
Nao viongozi wa Taasisi ya Benjamin Wiliam Mkapa walieleza azma ya harambee hiyo pamoja na chakula ikiwa ni pamoja na kuendeleza na kuimarisha sekta ya afya kwa upande wa Zanzibar na Tanzania Bara.
Naye Waziri wa Afya wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ummy Ally Mwalimu alieleza juhudi za makusudi zitakazochukuliwa na Serikali zote mbili kuiunga mkono taasisi hiyo.
Katika harambee hiyo jumla ya TZS Bilioni 1.2 zimepatikana, ambapo Rais Dk. Mwinyi alitoa shukurani kwa wachangiaji wote huku akiahidi kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar nayo haitokuwa nyuma katika kutoa mchango wake.
Imetayarishwa na Idaya ya Mawasiliano
Ikulu Zanzibar.
No comments:
Post a Comment