Na Oscar Assenga,TANGA.
HOSPITALI ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo imepokea msaada wa maabara ya kisasa ya kufanyia uchunguzi wa ugonjwa wa Uviko 19 yenye thamani ya Milioni 225 kutoka kwa Serikali ya Ujerumani kupitia Shirika lake la Maendeleo ya GIZ
Akizungumza mara baada ya kuifungua mara baada ya ukaguzi wa maabara hiyo Waziri wa Afya Ummy Mwalimu alisema kwamna maabara hiyo ina uwezo wa kutoa majibu ndani ya masaa nane hivyo kuwa mwarobaini wa changamoto zilizokuwepo awali.
Alisema kuwa pia kupitia uwepo wa maabara hiyo utasaidia hata wananchi kutoka nchi jirani ya Kenya ambao wataingia nchini kufanyiwa vipimo kwa haraka na majibu kupatikana kwa wakati.
Alisema uwepo wa maabara hiyo itaondoa changamoto iliyokuwepo ya kusafirtisha sampuli kwenda kwenye maabara nyengine ambapo ilikuwa inasababisha ucheleweshwaji wa majibu na wakati mwengine vipimo vilikuwa vinachelewa.
"Kwa niaba ya serikali tunawashukuru wenzetu wa Ujerumani kwa kutusaidia katika sekta ya Afya kama mnavyofahamu hospitali hii ilijengwa na wajerumani miaka 100 iliyopita lakini bado wanaendelea kutoa fedha nyingi katika kusaidia sekta ya afya nchini ikiwemo hospital yetu ya rufaa ya mkoa wa Tanga Bombo wanatupatia fedha kwaajili ya kuimarisha afya ya uzazi ,mama na mtoto pamoja na mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona "Alisema
Alisema kuzinduliwa kwa kituo hicho cha kupima sampuli za Corona kitasaidia na kuokoa muda kwani awali ilikuwa inawalazimu sampuli zinazochukuliwa hospital Bombo kwenda kupimwa Dar es salaam kwenye maabara ya Taifa na baada ya masaa 48 ndio majibu kupatikana ambapo sasa majibu yatakuwa yanapatikana ndani ya masaa 8 na kuwarahisishia wanaosafiri kwenda nje ya nchi kupata majibu kwa haraka zaidi.
Waziri Ummy alisema pia fedha walizitoa zitatumika kwaajili ya kuimarisha mapambano dhidi ya Uviko -19 na ndio maana katika hospitali ya rufaa ya mkoa Bombo wamefungua kituo cha kupima sampuli za Corona kwa kutumia kipimo hicho.
Awali akizungumza Waziri wa Ushirikiana wa Uchumi na Maendeleo kutok Serikali ya Ujerumani Dkt Barbel Kofler alisema kuwa wakazi wa Tanga pamoja na wageni kutoka nje sasa wataweza kutumia maabara hiyo kwa ajili ya vipimo vya UVIKO.
Alisema wanajisikia furaha kuona kituo hiki cha kupimia sampuli za Covid 19 kinaanza kufanya kazi kwaajili kuimarisha afya ya jamii ya watu wa Tanga na ni muhimu sana kwa serikali ya ujerumani kuendelea kusaidia sekta ya afya katika mapambano dhidi ya magonjwa mbalimbali ya mlipuko.
Alieleza kwa sababu wote hatuko salama muda wowote hivyo wanapaswa kushirikiana kusaidia katika kuimarisha afya ya jamii kwa ujumla kwa Tanzania na ulimwengu mzima pia
Dkt. Kofler alisema mbali na fedha hizo wamesaidia kuwajengea uwezo wataalamu wa afya katika kutoa huduma bora huku wakingia Dolla za kimarekani 15.3 kwaajili ya kusaidia afya ya mama na mtoto na wasichana ili kupambana, kupunguza au kutokomeza kabisa vifo vitokanavyo na uzazi.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa maabara kuu ya Taifa ya Afya ya Jamii Medard Beyanga alisema kuwa Serikali inaendelea kuziimarisha maabara zote hapa nchini kwaajili ya kupelekea huduma karibu na wananchi ambapo baadhi ya vituo hapa nchini vimeanza kufunguliwa ikiwemo kilichopo katika hospital ya rufaa mkoa wa Tanga Bombo.
Alisema kwamba hivi sasa wanaendelea na mpango wao wa kuziimarisha maabara za upimaji wa Uviko - 19 na Serikali inafanya jitihada za kuongeza upimaji ili kupeleka huduma karibu na wananchi kuliko kusubiri majibu kutoka Dar es salaam kwenda maabara kuu ya Taifa ,na hii maabara haitakuwa ya kupima Corona bali itapima na magonjwa mengine.
Aidha alieleza pia Serikali ya Ujerumani pia imeendelea kuwa na mchango mkubwa hapa nchini kupitia sekta ya afya ambapo inasaidia kulipia bima ya afya na mtoto inayotambulika kama 'Tumaini la mama', kuchangia mapambano dhidi ya kifua kikuu pamoja na malaria.
“Serikali ya Ujerumani imedhamini miradi ya afya ya Nchini Tanzania kwa gharama ya shilingi dola za kimarekani za zaidi ya shilingi bilioni 7 ikihusisha miradi ya mama na mtoto na Uviko 19”Alisema
No comments:
Post a Comment