Habari za Punde

Mhe Hemed akutana na Brigedia Jenerali wa Jeshi la Wananchi Tanzania kanda ya Zanzibar


 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amemtaka Brigedia Jenerali wa Jeshi la Wananchi Tanzania kanda ya Zanzibar Ndugu  Said Khamis Said kuimarisha ushirikiano na vyombo vengine vya ulinzi na usalama vilivyopo nchini.

Mhe. Hemed ameeleza hayo afisini kwake Vuga Jijini Zanzibar alipokutana na kufanya mazungumzo na Brigedia Jenerali Said alipofika kujitambulisha baada ya kushika wadhifa huo.

Ameeleza kuwa wananchi wa Zanzibar wana imani kubwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa kuwa ni  sehemu ya wananchi ambapo uwepo wao unasababisha wananchi kuishi bila ya hofu ya aina yoyote kwani wana jua kuwa nchi ipo katika mikono salama.

Aidha Mhe. Hemed amemtaka  Brigedia Jenerali said   kusimamia na kuongeza mashirikiano baina ya JWTZ na vyombo vyengine vya ulinzi na usalama ili kuhakikisha kuwa Tanzania inabakia salama.

Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema  Jeshi la Wananchi  tanzania ndio nguzo tegemezi nchini hivyo amemtaka Brigedia Jenerali Said kuhakikisha wanailinda miundo mbinu iliyopo nchini kwa maslahi ya wazanzibari na watanzania kwa ujumla.

Pia  Mhe. Hemed amemueleza Brigedia General, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dokta Hussein Ali Mwinyi itaendelea kushirikiana na Jeshi la Wananchi wa Tanzania ili kuwaletea maendeleo wananchi wake.

Pamoja na mambo mengine Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amemtaka Brigedia General Said Kukaa na wananchi na kuzungumza nao kwa kuondosha changamoto ndogo ndogo baina yao ili kuimarisha umoja na mashirikiano yaliyopo baina ya Jeshi  na wananchi.

Kwa upande wake Brigedia General Said Khamis Said amemuahidi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa ataendeleza mazuri yote  yaliyoachwa na waliomtangulia kwa lengo la kuhakikisha  Tanzania na mipaka yake yote inabakia salama muda wote.

Aidha Brigedia General Said ameahidi atahakikisha anailinda miundombinu iliyopo kwa mashirikiano na vyombo vyengine vya ulinzi na usalama akiwa kama mwenyekiti wa kamati hio Zanzibar Na kuhakikisha nchi inabakia kuwa salama muda wote.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.