Habari za Punde

Tuitumie Fursa ya Amani Iliyopo Kuitangaza Hazina ya Zanzibar Kupitia Mbio za Marathon.– Mhe.Othman.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman, (wapili kulia) akipiga Bastola juu kuashiria Kuanza kwa Mbio za Tigo-Zantel Zanzibar International Marathon za Kilomita 1,5,10,21 na Mbio za Baiskeli za Kilomita 38.3 katika Viwanja vya Forodhani, Mkoa wa Mjini- Magharibi Unguja, leo tarehe 07 Agost,2022.(Picha na Kitengo cha Habari Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar).
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman,(Mshiriki namba 003) akiwa pamoja na Viongozi mbali mbali wa Serikali, Vyama vya Michezo, Wafadhili na Taasisi binafsi katika Mbio za Tigo-Zantel Zanzibar International Marathon za Kilomita 5, kuliani kwake ni Mhe. Simai Mohamed Said (Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale), Mhe. Yahya Mamba (Mwakilishi wa Jimbo la Kwahani Mjini Unguja), na Bw.Hassan Zanga Mwenyekiti wa (Zanzibar International Marathon); Kushotoni kwa  Mheshimiwa Makamu ni Bw. Innocent Rwetabura (Kaimu Mkurugenzi Mkuu Tigo-Zantel), Mhe. Hamza Hassan Juma (Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar) na Idrisa Kitwana Mustafa (Mkuu wa Mkoa wa Mjini- Magharib Unguja). (Picha na Kitengo cha Habari, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar).
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman, akikabidhi zawadi ya Bahasha, yenye Fedha Taslim kiasi cha Shilingi milioni moja kwa Mshindi wa Kwanza wa Mbio za Baiskeli za Kilomita 38.3 za Tigo- Zantel Zanzibar International Marathon kwa upande wa Wanawake, Bi.Jamila Abdallah, ambaye ni Mshiriki kutoka Zanzibar, katika viwanja vya Forodhani, Mkoa wa Mjini- Magharibi Unguja, leo tarehe 07 Agosti, 2022.(Picha na Kitengo cha Habari Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar).
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman, akivalishwa Medali na Mwakilishi wa wadhamini wakuu wa Mbio za Tigo- Zantel Zanzibar International Marathon ambaye ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Tigo-Zantel, Bw. Innocent Rwetabura mara baada ya kukamilisha Mbio za Kilomita 5, zilizoanza na kumalizika katika Viwanja vya Forodhani, ambazo zimezunguruka katika maeneo mbali mbali ya Mkoa wa Mjini-Magharibi Unguja , leo tarehe 07 Agost,2022.(Picha na Kitengo cha Habari Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar).
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman, akizungumza na viongozi, wanamichezo, na wananchi, mara baada ya kukamilika kwa Mbio za Tigo-Zantel Zanzibar International Marathon za Kilomita 1,5,10,21 na Mbio za Baiskeli za Km 38.3 zilizoanza na kumalizika katika viwanja vya Forodhani, ambazo zimezunguruka katika maeneo mbali mbali ya Mkoa wa Mjini-Magharibi Unguja, leo Agost 07, 2022. (Picha na Kitengo cha Habari, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar).
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman, akizungumza na viongozi, wanamichezo, na wananchi, mara baada ya kukamilika kwa Mbio za Tigo-Zantel Zanzibar International Marathon za Kilomita 1,5,10,21 na Mbio za Baiskeli za Km 38.3 zilizoanza na kumalizika katika viwanja vya Forodhani, ambazo zimezunguruka katika maeneo mbali mbali ya Mkoa wa Mjini-Magharibi Unguja, leo Agost 07, 2022. (Picha na Kitengo cha Habari, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar).

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema kuwa Zanzibar International Marathon ni Tangazo muhimu la kuutangaza Utalii wa Nchi, mbele ya mataifa ulimwenguni.

Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo akiongoza Mbio za Tigo-Zantel Zanzibar International Marathon, huko Forodhani, Mkoa wa Mjini-Magharibi Unguja.

Amesema kuwa Zanzibar inayo hazina kubwa ambayo ni urithi wake wa asili, bali kwa mnasaba wa kufanyika kwa Mbio hizo kunaashiria uwepo wa hali njema ya amani, umoja, utulivu na mshikamano, ambayo inazidi kupamba uzuri na mandhari bora ya visiwa vya Unguja na Pemba.

Hivyo ameeleza kuwa Mbio hizo za Kimataifa ni fursa muhimu ya kuitangaza Zanzibar, ambayo ni Nchi yenye historia kubwa na vivutio vilivyopambwa na utamaduni bora unaogusa asiili za watu wa Mataifa mengi ulimwenguni.

Aidha, Mheshimiwa Othman   ametoa changamoto kwa Mamlaka kutumia fursa hiyo ya kila mwaka kuitangaza Zanzibar na Vivutio vyake, ukiwemo Mji Mkongwe wa Asili ambao pia ni sehemu ya Hifadhi ya Kimataifa, huku akitoa wito kwa Waandaaji ambao ni Zanzibar International Marathon, kufanya maandalizi mapema ili kufanikisha Marathon ijayo kuwa na ufanisi zaidi.

Pamoja na kushiriki Masafa ya Kilomita 5 ya Mbio hizo, Mheshimiwa Othman amekabidhi zawadi kwa  Washindi pamoja na kuwavisha Medali.

Viongozi mbali mbali wameungana na Makamu wa Kwanza wa Rais katika mbio hizo, ambao ni pamoja na Mstahiki Meya wa Jiji la Zanzibar, Mhe. Mahmoud Mohamed Mussa, Wairi wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Mheshimiwa Simai Mohamed Said, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanziibar, Mhe. Ali Abdulghulam Hussein na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja; Mhe. Idris Kitwana Mustafa.

Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanziibar, Mhe. Hamza Hassan Juma, amesema kuwa Michezo hiyo ni muhimu katika mwelekeo mzima wa kuitangaza Sekta ya Utalii na Nchi kwa ujumla wake.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Tigo-Zantel, Bw.  Innocent Rwetabura ameishukuru Serikali ya Zanzibar kwa kutoa fursa hiyo ya kukuza vipaji ambavyo ni mlango wa kuitangaza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania michezoni, katika medani za kimataifa.

Amesema hilo limethibiti hivi karibuni ambapo Mshindi wa  Tigo Kili Half Marathon iliyopita, Mtanzania Felix Simbu, ameipatia na kuitangaza Nchi baada ya kutwaa Medali ya Fedha, katika Mashindano ya Jumuiya ya Madola, yanayoendelea Jijini Birmingham Nchini Uingereza.

Tigo-Zantel Zanzibar International Marathon 2022, iliyohusisha pia Mbio za Baiskeli, Riadha kwa Watoto na Watu wenye Ulemavu, imewajumuisha washiriki kutoka Mataifa mbali mbali ya Jirani mwa Tanzania na Nje ya Bara la Afrika.

Kitengo cha Habari

Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar

Agost 07, 2022.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.