Habari za Punde

Utafiti ni Muhimu kwa Maendeleo ya Taifa – Dkt Mwinyi

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman , akizungunza katika ufunguzi wa Kongamano la 16 la Kimataifa la Jumuiya ya wanazuoni na watafiti wa Mambo ya Kale (PAN AFRICAN ARCHAELOGICAL ASSOCIATION – PAA), katika Ukumbi wa taasisi ya Utalii ya Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA), kilichopo Maruhubi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, leo tarehe 09.08.2022. Mhe. Othman alifungua Kongamano hilo kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi.
( Picha na Kitengo cha Habari  Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar).

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman, amesema kwamba ushirikiano baina ya Wataalamu na Watafiti mbali mbali, unahitajika hasa katika nyanja ya mafunzo na Teknolojia, maabara na vifaa pamoja na machapisho ili kuendeleza vyema kazi hiyo.

Mhe. Othman ameyasema hayo leo huko Ukumbi wa taasisi ya Utalii ya Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA), kilichopo Maruhubi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, katika hotuba aliyoisoma kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi, alipofungua Kongamano la kumi na sita la kimataifa  la Jumuiya ya Wanazuoni na Watafiti wa Mambo ya Kale (PAN AFRICAN ARCHAELOGICAL ASSOCIATION – PAA).

Amesema taaluma ya Mambo ya Kale na Urithi wa Utamaduni unagusa sekta zote za kiuchumi, Kijamii , kisiasa, Teknolojia, Mazingira yakiwemo  Magonjwa mbali mbali, na kwamba ni tegemeo kubwa la taifa  kuweza kufahamu nchi ilikotoka, ilipo sasa na inakokwenda kwani tafiti  zinatoa mchango mkubwa katika utekelezaji wa malengo yanayopangwa nchini.

Hivyo Mhe. Othman amewashauri watafiti kuwa msaada mkubwa kwa kutafsiri matokeo ya tafiti zao kwa kuyachapisha, sambamba na mapendekezo yao ya kuboresha maeneo  ya tafiti hizo kwa lugha nyepesi ili kwa pamoja iwe ni sehemu ya vivutio vya Utalii .

Mhe. Makamu amefahamisha kwamba hatua hiyo itasaidia kuimarisha matumaini ya Zanzibar, Tanzania na kwengineko Afrika, kuweza kupokea wataalii wengi zaidi  kama zilivyo nchi nyengine nyingi duniani na kuchangia kuongeza mapato ya taifa na hivyo kukuza uchumi kwa haraka.

Mhe. Othman amewakaribisha watafiti mbali mbali duniani, kufanya tafiti zao Zanzibar hasa katika masuala ya Akiolojia  ya baharini kwa kuzingatia kuwa Serikali ya awamu ya nane, moja ya sera yake muhimu ni Uchumi wa Buluu na kwamba utajiri wa Urithi uliopo baharini unaweza kutumika kama fursa muhimu ya kukuza sekta hiyo  hapa Zanzibar.

Mhe. Othman amefahamisha kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatoa kipaumbele katika masuala ya Utafiti wa namna hiyo, na ndio maana imeunda Wizara kamili inayoshughulikia mambo ya Kale, na kwamba ni fursa kwa wataalamu kufanya tafiti mbali mbali za aina hiyo hapa Zanzibar.

Aidha amewataka washiriki wa kongamano hilo kutoka nchi mbali mbali duniani, kutenga muda wao kutembelea vivutio mbali mbali  vya utalii vilivyopo Zanzibar na Tanzania kwa jumla na itasaidia kuona hali ya ukarimu na usalama mzuri  uliopo nchini Tanzania.

Pia amewaeleza kwamba kufanyika kwa kongamano hilo hapa Zanzibar iwe ni fursa muhimu kwa watafiti kubaini maeneo tofauti ya kufanyiwa utafiti, ili kwa kushirikiana na Wizara na Vyuo Vikuu waweze kufanya tafiti tofauti  ambazo zinahitajika kwa mchango wa maendeleo.

Mapema Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar Mhe. Simai Mohammed Said, amesema kwamba Serikali kupitia wizara yake ipo tayari kutoa mashirikiano yatakayohitajika, katika kufanikisha kufanyika tafiti mbali mbali zinazohusu mambo ya Kale Zanzibar.

Kongamano hilo  limehudhuriwa na washiriki mbali mbali kutoka nje ya Tanzania, wakiwemo Kenya, Uganda, Zimbabwe, Aljeria, Ethiopia, Botswana, Afrika Kusini, Zambia, DRC Congo, Senegal, Nageria, Mali, Moroco na Wenyeji Tanzania ikiwemo Zanzibar chini ya maandalizi ya mashirikiano baina ya Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar - (SUZA), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam - (UDSM), Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) pamoja na Wizara inayoshughulikia Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar. 

Kitengo cha Habari

Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar 

Agost 09, 2022

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.