Habari za Punde

Wizara na Wadau Wakutana Kutatua Tatizo la Watoto Mitaani

Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii Dkt. Zainab Chaula akipokea kitabu cha Mkurugenzi wa Taasisi ya Azaria Foundation Audax Abeli kinachoelezea maisha yake ya mtaani  chenye lengo la kuisaidia Jamii kuwaondoa watoto katika mazingira hatarishi. Wengine ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Amon Mpanju na wajumbe wa Menejimenti ya Wizara mara baada ya kikao cha Menejimenti Jijini Dodoma tarehe 22 Agosti, 2022.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Azaria Foundation Audax Abeli akieleza jambo wakati wa kikao ha Menejimenti ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kujadili namna ya kuwaondoa watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani, kilichofanyika Jijini Dodoma
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii Dkt. Zainab Chaula akiongoza kikao cha Menejimenti ya Wizara hiyo na Taasisi ya Azaria Foundation kujadili namna ya kuwaondoa watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani, kilichofanyika Jijini Dodoma

Na WMJJWM Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imejipanga kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha inapunguza tatizo la Watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani.

Akizungumza katika kikao naTaasisi ya Azaria Foundation jijini Dodoma Agosti 22, 2022 Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt Zainab Chaula ameitaka jamii kuwa na upendo kati ya familia na kuhakikisha watoto wanatunzwa katika familia ili wapate Malezi na Makuzi Bora katika ukuaji wao.

Dkt. Chaula amesema pamoja na kuwa mwanzilishi wa Taasisi hiyo ni zao la watoto walioishi mazingira magumu baada ya kutelekezwa na familia yake amekuwa msaada kwa watoto wengine ili wasiendelee kuishi maisha hayo.

"Familia inaposhindwa kwa namna yoyote ile, sisi Jamii tuchukue wajibu na tuungane na Wadau hawa kutatua shida hii, Wizara tumejipanga kwa kushirikiana na Wadau kutumia mbinu zote" alisema Dkt Chaula

Naye Mkurugenzi na mwanzilishi wa Taasisi ya Azaria Foundation, Audax Abeli ambaye ameishi maisha ya mtaani amesema familia yake ilikuwa chanzo cha yeye kuitwa Mtoto wa mtaani jina ambalo siyo sahihi hivyo namna bora ya kuwatoa watoto hao mtaani ni kuanzia upendo kwao.

 "Hili tatizo la watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani linatakiwa kushughulikiwa kuanzia ngazi ya mtaa hadi taifa, tunaweza tukapunguza watoto wa mtaani. Pia changamoto nyingine zinatokana na familia" alisema Audax.

Ameeleza kuwa mpaka sasa Taasisi hiyo inahudumia jumla ya watoto 70 kwa kuwapatia huduma muhimu za Kijamii na kuwapatia mbinu mbadala za kupambana na maisha.
 
Kwa upande wake Kamishna wa Ustawi wa Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Nandera Mhando amesema Wizara itashirikiana vyema na mdau wa Taasisi hiyo kwa kusaidiana na timu ya wataalamu inayofanya kazi ya kushughulikia watoto wanaoishi mazingira magumu na kuwatoa mtaani.

"Mojawapo ya mradi utakaozinduliwa hivi karibuni  ni mradi wa ujenzi wa kituo cha kupokea watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani na kuwapitisha katika mabadiliko ya tabia na ujuzi ili wanaporudi majumbani waweze kujiajiri" alisema Dkt. Nandera.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.