Habari za Punde

Imani za Wananchi Zinategemea Zaidi Kuwepo kwa Uadilifu wa Watendaji wa Vyombo Vinavyosimamia Utoaji wa Haki

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema utoaji wa haki ni muhimu katika maendeleo ya kiuchumi hapa nchini.

Dk. Mwinyi amesema hayo katika uzinduzi wa Ripoti ya mahitaji ya mfumo wa Mahakama Zanzibar pamoja na Ofisi ya Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC – ZANZIBAR), hafla iliofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip, iliopo Uwanja wa Ndege, Zanzibar.

Amesema imani za wananchi zinategemea zaidi kuwepo kwa uadilifu  wa watendaji wa vyombo vinavyosimamia utoaji wa haki, na akatumia fursa hiyo kubainisha uwepo wa watendaji wachache katika taasisi hizo wanaaojihusisha na vitendo vilivyo kinyume maadili na utawala bora.

Alitoa wito kwa Viongozi vya watendaji wa vyomvo hivyo kuwa makini na waadilifu katika utekelezaji wa majukumu yao ili wananchi waweze kujenga imani na vyombo hivyo.

Dk. Mwinyi alisema mafanikio ya kuchumi yanategemewa  sana kuwepo kwa misingi ya sheria pamoja na mfumo bora wa mahakama.

Aidha, alipongeza uamuzi wa kufungua Ofisi za Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu hapa Zanzibar na kusema hatua hiyo itaongeza kasi ya mafanikio katika utekelezaji wa shughuli zake.

Katika hatua nyengien, Dk. Mwinyi alisema Serikali imeanza kuchukua hatua za kuboresha Idara ya Mahakama, (hata kabla ya ripoti hiyo kutayarishwa), ambapo imeanzia na ngazi ya  Mahakama Kuu, lengo likiwa ni kuimarisha utendaji.

Alisema maboresha hayo yanahusisha eneo la rasilimali watu, rasilimali fedha, mfumo wa Mtandao pamoja na upatikanaji wa vifaa na zana muhimu za kutendea kazi, ikiwemo vyombo vya usafiri.

Alitoa shukrani kwa viongozi na watendaji wa Idara hiyo kwa utendaji bora wa kazi mbali na kukabiliwa na  changamoto mbali mbali katika utekelezaji wa majukumu yao.

Nae, Jaji Mkuu wa Zanzibar Khamis Ramadhan Abdalla alisema ripoti hiyo itatumika kwa ajili ya kuandaa mpango kazi wa miaka mitano, lengo likiwa ni kuwa na mahakama inayowajibika ili hatimae wananchi waweze kujenga imani nayo.

Alisema bado kuna tatizo kubwa la jamii kushindwa kufika mahakamani kutoa ushahidi, hususan katika kesi za Udhalilishaji pamoja na upatikanaji/usafirishaji na matumizi ya Dawa za kulevya, na akatumia fursa hiyo kutoa wito kwa Wakuu wa Mikoa na  Wilaya kote nchini kusaidia kuihamasiaha jamii kubadili mitazamo.

“Vyobvo vya sheria ikiwemo Ofisi ya DPP pamoja na ZAECA wajipange vyema kuhusiana na kesi wanazofikisha mahakamani, wahakikishe zinakuwa na mashahidi, ili kuwepo mafanikio kunahitajika mashirikanao kati ya vyomvo vyote na wadau wa mahakama”, alisema.

Mapema, Waziri wa Nchi (OR) Sheria, Katiba na Utawala Bora Haroun Ali Suleiman alisema Wizara inalenga kujenga mahakama za kisasa za ngazi mbali mbali  katika Mikoa yote nchini, ili kuwawezesha watendaji kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Alisema Wizara itaiangalia ripoti hiyo kwa makini na kutekeleza yale yote yalio ndani ya uwezo wa Serikali ili kuwawezesha watendaji kufanya kazi zao katika mazingira bora zaidi.

 

Wakati huo huo; Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi alishirki katika mazishi ya Askofu Mkuu mstaafuJohn Aukland Ramadhan yaliofanyika Kanisa la Anglican Mkunazini, Mkoa Mjini Magharibi.

 

Katika hafla hiyo, iliohudhuriwa na Viongozi mbali mbali wa kitaifa, wakiwemo Mawaziri kutoka SMZ na SMT, Waziri wa Nchi (OMPR) Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi Hamza Hassan Juma alitoa salamu za rambirambi kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kusema wakati wa uhai wake Hayati Askofu John Ramadhan alitoa mchango mkubwa katika kuleta ustawi wa Taifa.

 

Alisema Hayati Askofu Ramadhan alishirikiana kikamilifu na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Viongozi mbali mbali katika kuhimiza na kusimamia amani nchini.

 

Waziri Hamza alisema ana matumaini makubwa kuwa Kanisa litayaendeleza yale yote aliyoyaasisi na akatumia fursa hiyo kutoa mkono wa pole kwa familia na Kanisa Anglican kwa ujumla.

 

Hayati Askofu Mkuu mstaafu John Ramadhan, mwenye umri wa miaka 90,  alifariki dunia Septemba 12, 2022 katika Hospitali ya Taifa  Muhimbili alikokuwa amelezwa kwa vipindi tofauti.

   

Imetayarishwa na Idaya ya Mawasiliano

Ikulu Zanzibar.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.