Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Amekutana na Kuzungumza na Mabalozi Watanzania Wanaokwenda Nchi za Zimbabwe, Zambia na Uholanzi

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na  mabalozi ambao wanakwenda kuiwakilisha Tanzania katika nchi za Zimbabwe, Zambia pamoja na Uholanzi waliofika kwa ajili ya kujitambulisha na kumuaga baada ya kushika Wadhifa huo Ofisini kwake Vuga.

Na.Ali Mohammed. OMPR.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amewahakikisha ushirikiano wa hali ya juu mabalozi ambao wanakwenda kuiwakilisha Tanzania katika nchi za Zimbambwe, Zambia pamoja na Uholanzi.

Ameyasema hayo katika mazungumzo yaliyofanyika Afisini kwake Vuga Jijini Zanzibar wakati alipokutana na  mabalozi hao waliofika kwa ajili ya kujitambulisha na kumuaga baada ya kushika Wadhifa huo.

Mhe. Hemed amewataka mabalozi hao kwenda kuimarisha ushirikiano uliopo baina ya nchi ambazo wanakwenda kuiwakilisha Tanzania kwa kutumia mfumo wa kisasa kwa maslahi ya watanzania kwa ujumla.

Aidha amewataka mabalozi hao kwenda kuangalia fursa za kiuchumi zilizopo katika nchi wanazokwenda kuitumikia Tanzania ili kuweza kuzifanyia kazi kwa lengo la kupata maendeleo endelevu.

Makamu wa Pili wa Rais amewataka mabalozi hao kuzitumia fursa  za uwekezaji zilizopo Nchini na kuwakaribisha Wawekezaji kuja kuwekeza ili kukuza Uchumi wa Nchi pamoja kuitangaza Zaidi Tanzania.

Mhe. Hemed ametumia fursa hiyo kuwaasa mabalozi hao kuitangaza Tanzania kwa mazuri yake hasa Suala la Utalii na vivutio mbali mbali vilivyopo Nchini ili kukuza Sekta ya Utalii pamoja na kukuza pato la taifa.

Sambamba na hayo Mhe. Hemed amewataka mabalozi hao kuamini kuwa watanzania wote wanawategemea kupitia nchi ambazo wanakwenda kuiwakilisha Tanzania ili wananchi  kuweza kupata manufaa kupitia wao.

Akizungumza kwa niaba ya mabalozi wenzake balozi ambae anakwenda kuiwakilisha Tanzania nchini Zambia Luteni General Mathew E.Mkingule  amemuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa watahakikisha wanayatekeleza kwa vitendo yale yote ambayo wameagizwa na viongozi kwa maslahi ya watanzania wote.

Aidha Balozi Mkingule ameeleza kuwa watahakikisha lolote ambalo wanalifanya watafanya kwa maslahi ya watanzania huku wakiwa na kaulimbiu ya kuwa jamuhuri ya muungano kwanza.

Mabalozi waliokutana ni pamoja na malozi amaekwenda kuiwakilisha Tanzania nchini Zimbabwe IGP Mstaafu Simon Nyakoro Sirro

Balozi anaekwenda kuiwakilisha Tanzania nchini Zambia Luteni general Mathew E. Mkingule

Balozi anaekwenda kuiwakilisha Tanzania nchini Uholanzi Bi Caroline Kitana Chipeta

Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

23/09/2022

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.