Habari za Punde

KIST yakaribisha wanafunzi wapya


 Mkuu wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume  Zanzibar  (KIST), Dk. Mahmoud Abdulwahab akizungumza na Wanafunzi wapya waliojiunga na  Taasisi ya  Karume katika wiki ya kuwakaribisha (Orientation week), hafla iliyofanyika  Ukumbi wa Mkutano wa Dk. Idrissa Muslim Hija katika Taasisi hiyo Mbweni Zanziabar.

Picha na Maryam Kidiko - KIST.

Na Issa Mzee   - KIST           28/10/2022.

Mkuu wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume Zanzibar (KIST), Dkt. Mahmoud Abdulwahab Alawi, amewasisitiza Wanafunzi wapya waliopata nafasi za masomo katika Taasisi hiyo, kufuata sheria na taratibu za Taasisi ili waweze kutimiza malengo yao.

Alisisitiza hilo wakati akizungumza na Wanafunzi katika wiki ya kuwakaribisha Wanafunzi wapya, katika Ukumbi wa Mkutano wa Dkt. Idrissa Muslim Hija Mbweni Zanzibar.

Dkt Mahmoud alisema endapo wanafunzi hao watafuata sheria na taratibu zilizowekwa na Taasisi, wataweza kupata elimu iliyobora na kufanikisha malengo yao yaliyowaleta katika Taasisi .

Alisema kumekuwa na baadhi ya Wanafunzi ambao wanabahatika kupata nafasi ya masomo katika Taasisi ya Karume, lakini kutokana na tabia ya ukiukwaji wa sheria inapelekea kukosa elimu waliokusudia na hatimae kushindwa kutimiza malengo yao.

“Nawasisitiza Wanafunzi wetu wapya kufuata sheria na taratibu zetu tulizoziweka hasa  sheria za mitihani, kwani ikiwa sheria hizi mutazifuata mutaweza kuwa wataalamu wazuri hapo baadae” alisema Mkuu wa Taasisi.

Katika hatua nyengine , Dkt. Mahmoud aliwasisitiza na kuwashauri Wanafunzi kuwa wavumilivu na kutokata tamaa katika kipindi hiki cha masomo, kwani wengi kati yao wamekutana na mazingira mapya yenye mchanganyiko wa watu tofauti.

“Hiki ni kipindi muhimu katika maisha yenu, hivyo kuweni wavumilivu na mukitumie vizuri ili muweze kubadilisha maisha yenu badae kutokana na elimu mutakayoipata hapa” alisema Dkt. Mahmoud.

Aidha aliwasisitiza Wanafunzi hao kuwa na nidhamu ya hali ya juu kipindi cha masomo pamoja na kutekeleza majukumu yao, ikiwemo ulipaji wa ada kwa wakati ili kuendeleza utoaji wa huduma kwa wakati.

Kwa upande wao Wanafunzi walishukuru Uongozi wa Taasisi kwa mapokezi mazuri na kuuomba Uongozi uzidi kuwapa nafasi ya kutosha ili waweze kukamilisha taratibu za malipo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.