Habari za Punde

Naibu Katibu Mkuu Mkomi Asisitiza Ushirikiano Katika Kulinda Shoroba za Wanyamapori

 Naibu Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Juma S. Mkomi akizungumza wakati wa kikao kazi cha Wataalamu mbalimbali wa Wizara za kisekta ambapo amesema jukumu la ulinzi wa shoroba ni letu sote.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Juma S. Mkomi amesema ushirikiano kati ya Wizara za Kisekta ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha shoroba za wanyamapori haziendelei kuharibiwa
 
Ametoa kauli hiyo leo tarehe 8 Oktoba, 2022 wakati allipokuwa akizungumza kwenye kikao kazi cha Wataalamu waliokutana Jijini Arusha kwa lengo la kujenga uelewa wa pamoja na kujadili utekelezaji wa Mpango Kazi wa Kuongoa Shoroba za Wanyamapori
 
‘’Jukumu la ulinzi wa shoroba za wanyamapori ni letu sote kwa maana ya Wizara zetu za kisekta ambazo zinagusa masuala ya Uhifadhi zikiwemo Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ofisi ya Rais- TAMISEMI, Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Ujenzi na Uchukuzi, Maji, Mazingira na nyinginezo ’’ amesema Naibu Katibu Mkuu, Mkomi
 
Amefafanua kuwa kikao kazi hicho cha  Watalaam ni moja ya hatua muhimu itakayosaidia Wizara zinazohusika na uanzishwaji na usajili wa vijiji, ujenzi wa miundombinu, shughuli za kilimo pamoja ufugaji kuwa na uelewa wa pamoja katika kutekeleza mpango kazi wa kuongoa shoroba hapa nchini.
 
‘Kikao kazi  hiki ni muhimu kwa kuwa kimewaleta wadau kutoka katika sekta mbalimbali mtambuka ambazo zina mchango wa moja kwa moja katika kuhakikisha shoroba za wanyamapori zinalindwa na kuhifadhiwa ‘ amesisitiza Mkomi.
 
Awali, Mkurugenzi wa Wanyamapori, Dkt.Maurus Msuha amesema kuwa jitihada za makusudi za kulinda shoroba  zitasaidia kupunguza migongano iliyopo kati ya binadamu na  wanyamapori hususani tembo.

'Tunalinda wanyamapori hawa kwa ajili ya manufaa ya wananchi hivyo hatupendi kuona wananchi wanapata madhara kwa sababu tu wamejenga katika mapito ya wanyamapori hivyo ni lazima tuje na suluhisho la kudumu ili wananchi wasiendelee kupata madhara yanayoweza kuepukika" amesisitiza Dkt. Msuaha
 
Kwa upande wake,Mkurugenzi Msaidizi  kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu - Bunge na Siasa, Lina Kitosi amesema kuwepo kwa shughuli za kibinadamu katika maeneo husika, kunasababisha wanyamapori wasiweze kuhama kutoka eneo moja kwenda jingine hali ambayo inachangia kwa kiwango kikubwa kuongezeka kwa migongano baina ya wanyamapori .
 
"Kuwepo kwa shughuli za kibinadamu katika maeneo husika, kunasababisha wanyamapori wasiweze kuhama kutoka eneo moja kwenda jingine hali ambayo inachangia kwa kiwango kikubwa kuongezeka kwa migongano baina ya wanyamapori na binadamu" amesisitiza

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.