Habari za Punde

Mfumko wa bei za bidhaa na huduma kwa wananchi ni suala mtambuka ambalo huchangiwa na sababu nyingi zikiwemo mfumko wa bei ulimwenguni

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Waandishi wa Habari na Wahariri wa vyombo vya Habari, ikiwa ni muendelezo wake wa kuzungumza na Waandishi kila mwisho mwa mwezi, mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar leo 31-12-2022.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi alisema tatizo la mfumko wa bei za bidhaa na huduma kwa wananchi ni suala mtambuka ambalo huchangiwa na sababu nyingi zikiwemo mfumko wa bei ulimwenguni kutokana na mabadikilo ya dunia ikiwemo vita vya Urusi na Ukrain sambamba na changamoto zinazobasabishwa na ufinyu wa bandari ya Zanzibar.

Alisema kupanda kwa bei za bidhaa sio tatizo liliopo Zanzibar pekee lakini ametolea ufafanuzi kwa sababu zilizo ndani ya mamlaka za serikali kuchukuliwa hatua za haraka ili kupunguza ukali wa maisha ikiwemo kuboresha ufanisi na utendaji wa utoaji huduma kwenye bandari ya Zanzibar ili kupunguza athari kali kwa wananchi.

Dk. Mwinyi aliyasema hayo wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari kwenye mkutano wake na waandishi hao anaoufanya kila mwisho wa mwezi kwa kuzungumza nao pamoja na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini.

“Kuhusu kupanda kwa bei za bidhaa, nataka niseme kwamba ziko sababu nje ya uwezo wa Serikali hatuna jinsi, zikiwemo kupanda kwa bei za bidhaaa huko zinakotoka, kuna baadhi ya mataifa wamezuia kuuza bidhaa zao nje ya nchi kwaaajili ya kujiwekea akiba kutoka na vita wa Urusi na Ukrain hali iliyochangia kupungua kwa uingizwaji wa bidhaa nchini, hayo na mengine ndio yanayosababisha bidhaa za chakula duniani kupanda sio Zanzibar peke yake” alifafanua Dk. Mwinyi.

Akizungumzia mfumko wa bei kwa bidhaa za Zanzibar, Dk. Mwinyi alieleza bidhaa nyingi za vyakula zinatoka Tanznaia bara ambako pia bidhaa zimepanda bei kutokana na ukame ulioikumba baadhi ya mikoa nakuongeza kuwa ukame umepunguza uingizwaji wa bidhaa na kusababisha bidhaa chache ziliopo kupanda bei sambamba nakueleza changamoto zinazisababishwa na bandari ya Zanzibar ikiwemo ufinyu wa mazingira ya bandari ya malindi hali aliyoielezea kuchangia kuzorotesha zoezi la kushushwa kwa mizigo bandarini hapo.

“Bandari yetu ufanisi wake ni mdogo sana, sababu ina gati moja, meli zinakuja zinakaa sana, zikifuatana meli tatu nne, wa mwisho atashusha mzigo baada ya mwezi mmoja” alibainisha Rais Mwinyi.

Alisema, Serikali imechukua hatua ya kupunguza baadhi ya changamoto ikiwemo kutumia bandari ya Mangapwani ili kupunguza msongamano kwenye bandari ya Malindi na kutoa wepesi wa bidhaa nyingi kushushwa kwa wakati na kuwafikia wahitaji ambao ni wananchi.

Akizungumzia suala la maadhimisho ya sherehe za miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar Dk. Mwinyi alisema kwa mwaka 2023 hakutakua na sherehe kubwa badala yake gharama zilizopangwa kuadhimisha sherehe hizo zitaelekezwa kwenye miradi ya maendeleo ambapo Dk. Mwinyi alieleza fedha hizo zimepelekewa kuongeza nguvu Wizara ya Elimu.

Alieleza, awali sherehe za Mapinduzi zilipangwa kutumia milioni 700 licha ya gharama kupunguzwa hadi kufikia 450 milioni ambazo fedha hizo Rais Mwinyi alesema Serikali imezielekeza kuongeza nguvu kwenye miradi ya sekta ya Elimu ikiwemo kuongezwa kwa maradasa, madawati, maabara na huduma nyengine za elimu.

Kuhusu sekta ya Afya, Dk. Mwinyi alieleza katika kuboreshwa huduma za Afya kwenye vituo vya afya, Serikali imekuja na utaratibu mpya wa kutoa huduma kwa kushirikiana na sekta binafsi ili kuboresha huduma bora kwa wananchi nakuongeza kuwa Serikali kupitia hospitali za Wilaya na Mikoa zitatoa huduma zote na suala la huduma za maabara zimeelekezwa kwenye sekta binafsi ili kuipa wepesi serikali kuwahudunia zaidi wananchi.

“Sekta ya afya tumekuja na utaratibu mpya wa kutoa huduma zifanywe na sekta binafsi (outservices), kwa hivyo maabara za hospitali hizi mpya za wilaya na mikoa huduma zitatolewa na sekta binafsi, lile suala la mashine imeharibika sasa hivi hakuna tena, huduma zote za vipimo vya X -ray, MRI na huduma nyengine za kimaabara zimepelekwa huko” Alifafanua Dk.Mwinyi.

Kuhusu kutatua changamoto ya ajira nchini, Dk. Mwinyi alieleza tayari serikali imezungumza na balozi zake zilizo nje ya nchi ilikuangalia uwezekano wa kuwapata mawakala wa ajira na kuweka taratibu rasmi za ajira ili kukwepa lawama za baadae na ukiukwaji wa haki za binaadamu zinazovunjwa na baadhi ya waajiri kwa baadhi ya nchi.

“Tumeshazungumza na mabalozi wetu, watutafutie wale watu wanaoajiri  tuwaunganishe na mawakala wa huku ili vijana wetu waweze kufanyakazi nje” alifafanua Rais Mwinyi.

Rais Dk. Mwinyi, amekua akitumia utaratibu wa kuzungumza na waandishi na wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini ikiwa ni utaratibu wake wa kusikiliza na kutatua moja kwa moja changamoto zinazowakabili wananchi ambao baadhi yao humfikishia Mhe. Rais kupitia vyombo hivyo, na huu ni mkutano wa mwisho kwa mwaka 2023.

Imetayarishwa na Idara ya Mawasiliano

Ikulu Zanzibar.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.