Habari za Punde

Mhe Othman awaasa wajasiriamali kutangaza biashara zao ndani na nje

 

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman, amezitaka Taasisi za Mafunzo ya Amali, Watoa huduma, pamoja na Wajasirimali nchini kujitahidi kuzitangaza shughuli wanazofanya ili ziweze kufahamika vyema na jamii na watumiaji wengine mbali mbali wa ndani na nje ya nchi.

Mhe. Othman ametoa wito huo huko katika Viwanja Maisara mjini Zanzibar, alipotembelea mabanda mbali mbali ya maonesho ya Biashara ikiwa ni shamra shamra za sherehe za Mapituzi ya Zanzibar ya  Januari  1964 kutimiza miaka 59.

Mhe. Makamu amefahamisha kwamba zipo shughuli nyingi nzuri na zenye manufaa makubwa zinazofanywa na wajasiramali, utaalamu kutoka Taasisi za Elimu na pamoja na shughuli za watoa huduma lakini hazifahamiki ipasavyo kutokana na kutotangazwa vyema.

Amefahamisha kwamba kuwepo kwa maonesho hayo ni fursa muhimu za kutangaza na kuonmesha hatua kubwa za utaalamu na uzalishaji wa bidhaa zilizofikiwa kutoka taasisi mbali mbali nchini na kwamba kutangazwa ipasavyo kutasaidia vyema kueleweka na wenye mahitaji kuweza kuzitumia.

Aidha amezikumbusha taasisi za Elimu na hasa Vyuo vya Amali na na wazalishaji bidhaa za biashara kuzalisha bidhaa zenye kukubalika katika masoko ya ndani nanje  sambamba na kuzalisha wataalaum wanaokubalika na kukidhi matakwa ya soko hasa katika sekta ya Utalii inayoendelea kukua kwa kasi kubwa na mahitaji ya wataalamu kwa fani mbali mbali kuongezeka.

Akitembelea Banda la Utafiti wa Mifugo Mhe. Othman, ameshari Taasisi hiyo kujenga uwezo wa ndani kiutalam, ili  kuweza kuzalisha chakula cha mifugo ya aina mbali mbali inayohitajika hapa nchini.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti wa Mifugo Zanzibar Nd. Talib Ali Suleima, amesema kwamba malighafi nyingi zinazotumika kutayarisha na kuzalisha chakula cha mifugo ya aina mbali mbali zinatoka nje ya Zanzibar jambo ambalo linaongeza gharama kwa bidhaa hizo.

Naye Ofisa Mwandamizi wa kutoka Idara ya Utafiti wa Mifugo nchini Zuhera Karim Zam , amesema kwamba asilimia kubwa ya chakula cha mifugo kinatokana na bidhaa za kilo, huku wakulima wengi wa Zanzibar wakizalisha bidhaa chache na kulazimika kununa nje ya nchi jambo lonaloongeza gharama za bidhaa hizo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtedaji wa Mamlaka ya Vyuo vya Amali Zanzibar Dk. Bakari Ali Silima, amesema kwamba Mamlaka hiyo inawasiliana na watumaiaji wataalamu wa sekta ya Utalii ambao ni wamiliki wa mahoteli mbali mbali ili kueleza aina na haja ya wataalamu wanaowahitaji katika tasinia ya Hoteli nchini.

Amefahamisha kwamba kwa mujibu wa wamiliki hao, hoteli nyingi zinahitaji wataalamu wenye ujuzi mchanganyiko katika fani za utaalamu zaidi ya mbili ili waweze kuajirika na kutumika vyema kwenye ajira wanazopewa, jambo ambalo limezingatiwa ipasavyo na Mamlaka hiyo katika fani wanazofundisha nchini.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa MoroBatik Dk. Marieta Mkanga, ameiomba serikali kupunguza ama kuonsha kabisa kodi za bidhaa za batiki wanazotumia kuzalisha mashati, mikoba na magauni na bidhaa nyenginezo ili  uzalishaji wao uweze kuwa na gharama nafuu na kuweza kuhimili ushindani wa soko la ndani na nje kwa bidhaa za aina hiyo.

 

Imetolewa na Ofisi ya Makumu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kupitia Kitengo chake cha Habari Tarehe 11.01.2023

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.