Habari za Punde

Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar awataka Madiwani, Masheha na wananchi kubadili changamoto kuwa fursa

 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Mohammed Said Mohammed(Dimwa), akizungumza na Madiwani, Masheha, Wanachama na Kikundi cha Polisi Jamii Jimbo la Mpendae katika hafla ya kukabidhi vifaa vya ulinzi kwa kikundi hicho huko katika Afisi za Jimbo hilo Mpendae Zanzibar.leo Tarehe 30/01/2023
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Mohammed Said Mohammed(Dimwa),akisalimiana na baadhi ya viongozi wa Chama na Kikundi cha ulinzi cha Mpendae mara baada ya kuwasili katika Jimbo hilo katika hafla ya kukabidhi vifaa hivyo.
KIONGOZI wa Kikundi cha Polisi Jamii Shehia ya Bitihamran Da/Insp. Abdalla Muhsin (kulia)akikabidhiwa radio maalum za mawadiliano zenye uwezo wa kuwasiliana kwa zaidi ya masafa ya kilomita nne na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Mohammed Said Mohammed(kushoto), katika hafla iliyofanyika Jimbo la Mpendae.

NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.

NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Mohammed Said Mohammed (Dimwa),amewataka Madiwani,Masheha na Wananchi wa jimbo la Mpendae waunge mkono juhudi za vijana (Polisi Jamii) wanaojitolea kufanya kazi ya ulinzi katika maeneo ya Jimbo hilo.

Wito huo ameutoa leo wakati akikabidhi vifaa vya ulinzi, ambavyo ni redio maalum za mawasiliano kwa vijana hao ikiwa ni sehemu ya utekelezwaji wa ahadi yake.  

Dkt. Dimwa alisema masuala ya ulinzi na usalama wa jimbo hilo yanawagusa wananchi wote hivyo panapotokea vijana walioamua kujitolea bila kudai malipo wanatakiwa kuthaminiwa.

Alieleza kwamba Jimbo hilo kwa muda mrefu limekuwa na changamoto ya vitendo vya uhalifu mbali mbali unaofanywa na baadhi ya watu wasiokuwa na maadi, ambapo changamoto hiyo itatatuliwa kwa ushirikiano baina ya wananchi na Polisi Jamii hao.

Kupitia kikao hicho Naibu Katibu Mkuu huyo, alisema kuwa changamoto nyingine inayotakiwa kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu ni suala la kulinda na kutunza miundombinu ya Skuli ya msingi ya kisasa ya Salim Turky iliyojengwa na SMZ chini ya ufadhili wa mfuko wa Uviko-19 kupitia Shirika la Fedha Duniani(IMF) iliyofunguliwa hivi karibuni ili itoe huduma bora za kielimu kwa watoto wa jimbo hilo.

“Wananchi wenzangu wa Jimbo hili tunayotakiwa kujitoa na kujitolea zaidi katika masuala ya kijamii ili kubadili changamoto mbalimbali ziwe ni fursa ya mafanikio.”, alisisitiza Naibu Katibu Mkuu huyo Dimwa.

Katika maelezo yake Dkt. Dimwa aliwasihi Polisi Jamii hao kuendelea kujitolea kwa kufanya ulinzi katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo huku wakishirikiana na jamii husika kwani Jeshi la Polisi pekee haliwezi kumaliza vitendo hivyo.

Pamoja na hayo amekitaka kikundi hicho cha ulinzi kuandaa bajeti ya mahitaji yao ili aendelee kuwaunga mkono kadiri uwezo wa kifedha utakavyoruhusu.

Naye Kiongozi wa Polisi Jamii katika Shehia ya Bitihamran Da/Insp. Abdalla Muhsin, mara baada ya kukabidhiwa vifaa hivyo aliahidi kuvitumia kwa malengo yaliyokusudiwa.

Akitoa neno la shukrani Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Jimbo hilo Ndg. Abass Himid Yussuf, alimshukru Naibu Katibu Mkuu Dkt. Dimwa kwa maamuzi yake mazuri ya kutoa vifaa hivyo vitakavyosaidia mawasiliano katika kuimarisha ulinzi.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.