Habari za Punde

Rais Mhe Samia awapongeza vijana wa Kitanzania kwa kupata medali ya Fedha *Ni baada ya kuibuka washindi wa pili katika mashindano ya ubunifu duniani

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na vijana wa Kitanzania waliobuni roboti ya kukamata hewa ukaa (Carbon dioxide), ambapo walioshika nafasi ya pili kwenye mashindano ya ‘Global Robotic Challange’ , yaliyofanyika nchini Geneva Uswisi na kujumuisha zaidi ya Mataifa 190, kwenye Ukumbi wa Ofisi Ndogo za Waziri Mkuu Magogoni Jijini Dar es Salaam Januari 15, 2023.

                                                          (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) 

MHESHIMIWA Rais Dkt. Samia Suluhu Hssan amewapongeza vijana wa Kitanzania walioibuka washindi wa pili na kupata medali ya fedha katika mashindano ya kwanza ya Global Robotics Challenge yaliyofanyika Geneva Uswisi na kushirikisha mataifa zaidi ya 190. 

Amefarijika kusikia kuwa roboti iliyoundwa na vijana kutoka Tanzania chini ya maudhui ya kukamata hewa ukaa (Carbon dioxide) inaweza kusaidia kusafisha kaboni hewani na kusaidia kupunguza ongezeko la joto kwenye angahewa ya Dunia.

Kauli hiyo imetolewa leo (Jumapili, Januari 15, 2023) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia katika hafla ya kuwapongeza vijana hao iliyofanyika kwenye ukumbi wa Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es Salaam.

Amesema hayo ni mafanikio makubwa na Watanzania wote wanapaswa kujivunia kwa kuiwakilisha nchi yetu vizuri. “Nitumie nafasi hii kuwaahidi kuwa Serikali kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari itaendelea kufuatilia maendeleo yenu na kuona namna ya kuendeleza vipaji vyenu. ”

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuielekeza Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari iandae mpango wa kuwa na vituo vya ubunifu nchini katika ngazi za Mikoa na Wilaya mbalimbali ili kusaidia kuinua vipaji vya vijana.

Amesema Wizara iimarishe utaratibu wa kuwatambua na kuwaendeleza wabunifu mbalimbali ili kuwamotisha na kukuza ajira nchini na ishirikiane na mamlaka husika kuandaa utaratibu wa kuwasaidia wabunifu mbalimbali na kuwaunganisha na taasisi pamoja na makampuni kwa ajili ya kuendeleza bunifu za kazi zao kulingana na mahitaji.

Vilevile Waziri Mkuu ameielekeza Wizara hiyo na mamlaka husika zijipange kuwekeza katika kulinda usalama wa taarifa za watumiaji wa mifumo mbalimbali ya TEHAMA sambamba na  kutoa elimu kuhusu usalama sahihi wa vifaa na matumizi salama ya mifumo ya kompyuta.

Amesema Wizara hiyo kupitia Tume ya TEHAMA ifanyie kazi vikwazo mbalimbali vya kisera na kikodi vinavyoleta changamoto kwa wabunifu katika masuala ya TEHAMA na matokeo ya bunifu mbalimbali yawekewe utaratibu wa  kubidhaishwa/kupata soko badala ya kuwekwa maktaba.

Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ameipongeza Kampuni ya Mawasiliano ya Tigo kwa kuamua kutumia sehemu ya mapato yao kwa kuwasaidia vijana wa kike nchini katika kuendeleza bunifu nchini kupitia APPS and Girls.

Waziri huyo mesema kuwa takwimu mbalimbali zinaonesha kuwa ushiriki wa mabinti na wanawake katika matumizi ya TEHAMA si mzuri sana, Barani Afrika asilimia 24 tu ya wanawake wanashiriki kwenye TEHAMA huku wanaume ni asilimia 35.

Tanzania ukienda mashuleni watu wanaosoma Computer Science na mambo yanayohusiana na TEHAMA wanawake ni asilimia 10 tu, ni muhimu kuendelea kuongeza nguvu katika kupunguza pengo hilo. ”

Naye, Afisa Mkuu wa Udhibiti Kampuni ya MIC Tanzania PLC (TIGO), Innocent Rwetabula amesema kampuni yao inafanya kazi kwa kuzingatia vipaumbele vya Serikali kwa sekta ya mawasiliano na kuongoza safari ya kidigitali hadi kufikia Tanzania ya kidigitali.

Amesema uwezeshaji wa wasichana ni mojawapo ya programu zao kuu za uwajibikaji kwa jamii kwa lengo la kuwawezesha wasichana walio katika shule za sekondari na wale walioacha shule kwa sababu mbalimbali wenye umri wa kuanzia miaka 12 hadi 24 kupata ujuzi wa kidigitali na stadi za ujasiriamali.

Amesema lengo la ufadhili huo ni kuziba pengo kati ya wavulana na wasichana katika sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM), kutoa ujuzi na stadi za ujasiriamali kupitia utoaji wa mafunzo ya TEHAMA, ushauri na uanzishaji wa biashara mpya za kiteknolojia ambapo mwaka jana wasichana 1,590 walinufaika na mpango huo.

Akizungumzia kuhusu shindano la kwanza ya Global Robotics Challenge amesema hufanyika kila mwaka kwa mtindo wa Olimpiki na kauli mbiu ya mwaka huu ilikuwa ni cabon capture, ambayo ni mchakato wa kukamata hewa ukaa iliyopo na kuzuia isiingie angani. Kundi la wanafunzi watano kati ya 11 waliiwakilisha nchi na kupata nafasi ya pili.

Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake, Maria Mtega ambaye anasoma kitado cha pili shule ya sekondari ya St.Theresa amesema anashukuru kwa mafunzo waliyoyapa ambayo yamewezesha kupata nafasi ya pili na pia wataendeleza vipaji vyao na hatimaye waweze kuwa wabunifu wakubwa nchini.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

JUMAPILI, JANUARI 15, 2023.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.