Habari za Punde

Serikali Yatoa Bilioni 60 Kuanza Utekelezaji wa Ujenzi kwa Kiwango cha Lami Barabara ya Likuyufusi - Mkenda

 

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas akizungumza wakati anakagua moja ya miradi ya barabara inayotekelezwa mkoani Ruvuma katika kiwango cha lami.
Baadhi ya maeneo ya barabara ya Likuyufusi -Mkenda inayokwenda hadi Mkenda mpakani mwa Tanzania na Msumbiji kupitia wilaya ya Songea mkoani Ruvuma yenye urefu wa kilometa 124.

SERIKALI ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imetoa shilingi bilioni 60 kuanza ujenzi barabara ya lami kilometa 60 kutoka Likuyufusi  Kwenda Mkenda Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma.

Barabara hiyo ni ya mpakani mwa Tanzania na Msumbiji yenye urefu wa kilometa 124 ambayo ina Kwenda hadi katika daraja la Mkenda Mto Ruvuma mpakani mwa Tanzania na Msumbiji.

Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma Mhandisi  Ephatar Mlavi amesema serikali kwa kuanzia inatekeleza mradi huo kwa kilometa 60  kuanzia  Likuyufusi Manispaa ya Songea hadi Mkayukayu Halmashauri ya Wilaya ya Songea.

“Mradi huu utahusisha ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami, sehemu ya Likuyufusi – Mkayukayu yenye urefu wa kilometa 60’’,alisema Mhandisi Mlavi.

Hata hivyo amesema Zabuni ya mradi huo imeshatangazwa na imefunguliwa kuanzia Januari 2023 na kwamba utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuanza wakati wowote baada ya hatua stahiki za manunuzi kukamilika.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Songea Mheshimiwa Pololet Mgema kwa niaba ya wananchi wa wilaya hiyo,amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za kutekeleza mradi huo  ambao unaunganisha Tanzania na Msumbiji kwa barabara ya lami.

Amesema barabara hiyo itafungua fursa za biashara na uwekezaji kwa nchi mbili za Tanzania na Msumbiji  na kwamba wafanyabiashara na wawekezaji wataweza Kwenda katika nchi hizo kuangalia fursa mbalimbali zilizopo.

Baadhi ya wananchi wanaoishi kando kando mwa barabara hiyo wamesema kwa miaka mingi barabara hiyo  katika sekta ya usafiri na usafirishaji imekuwa kero kubwa hasa wakati wa masika kutokana na ubovu wa barabara.

Kwirinus Mapunda Mkazi wa Litapwasi amesema wananchi wanatarajia makubwa mradi huo utakapokamilika kwa sababu vyombo vya usafiri vitaongezeka hivyo kupunguza gharama za usafiri.

Amesema katika eneo la Muhukuru  kuna mgodi wa makaa ya mawe ambao Mwekezaji alishindwa kufanya kazi ya kuingiza magari ya kubeba makaa ya mawe kutokana na ubovu wa barabara hivyo amesema barabara hiyo ikiwekwa lami itaongeza wawekezaji ambao pia wataongeza ajira kwa wananchi.

Serikali imetenga shilingi bilioni 46.35 kwa ajili ya kuboresha sekta ya barabara mkoani Ruvuma katika bajeti ya  mwaka 2022/2023 .

Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma

Januari 17, 2023

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.