Habari za Punde

Tuwatunze Wazee

 

Na Maulid Yussuf

Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mhe Riziki Pembe Juma amewataka wananchi kuwatunza wazee popote walipo kwani ndio hazina kwa Taifa.

Mhe Riziki ameyasema hayo baada ya kula chakula cha mchana pamoja na Wazee wanaoishi katika Makao ya Wazee wasiojiweza wa Welezo na Sebleni, hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Wazee hao Welezo Mjini Unguja ikiwa ni miongoni mwa kuadhimisha miaka 59 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Amesema kwa namna yeyote utakavyomjali mzee, basi na wao muda utakapofika  Uzee nao watajaliwa ikiwa na ndugu, jamaa, familia na hata Serikali.

 " Uzee na kuzeeka haukwepeki,  ikiwa bado upo hai na umri unasogea uzee utakufika tu" amesema Mhe.Riziki.

Amesema kula chakula pamoja na wazee hao katika siku hii ni ahadi waliyoitoa Wizara ya kuwa watafanya hafla hiyo kabla ya sherehe za Mapinduzi kufika, ahadi ambayo waliitoa wakati walipowatembelea wazee hao hivi karibuni.

Mhe Riziki ametumia nafasi hiyo kuwashukuru Mamlaka inayosimamia masuala ya utoaji wa Bima Tanzania TIRA, kwa kuiunga Mkono  Wizara  kufanikisha ahadi hiyo.

" Mimi ni mwana chama wa chama cha Mapinduzi, na chama changu kinapokuwa kinatoa ahadi, kinatimiza. Kama tulivyomuona Rais wetu Dkt Hussein Mwinyi naye ni CCM, aliwaahidi wanafunzi watakaopata division one kwa kidatu cha nne na cha sita, atawapa laptop, na leo tarehe 11 January ahadi hiyo ameitimiza." Amesisitiza mhe Riziki. 


Naye Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto bi Abeida Rashid Abdallah ameishukuru Mamlaka ya TIRA kwa kusaidia Wizara katika kutimiza ahadi yake ya kula hakula pamoja na wazee.

Pia bi Abeida amechukua nafasi hiyo kumshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi kwa kuendelea kuwaenzi na kuwatunza wazee.

Kwa upande wake Meneja wa usimamizi wa Bima Tanzania TIRA, Bwana Mohamed Ameir amesema Mamalaka yao inaendelea kusimamia masualabya utoaji wa bima katika masuala mbalimbali na kuhakikisha inawatunza wazee kwa kuwa na siha njema kwa jamii.

Mmoja wa Wazee wanaoishi katika Makao ya wazee wasiojiweza Welezo mzee Mtoro Seif akitoa shukurani kwa niaba ya Wazee wote ameishukuru Wizara ya Maendeleo ya Jamii pamoja na kumuombea dua Serikali izidi kutekeleza yale yote iliyojipangia ikiwemo kuwaenzi wazee.

Katika hafla hiyo Mhe Riziki amewazawadia wazee wote kanga pamoja na vikoi ikiwa ni miongoni mwa sadaka yake kwa wazee hao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.