Habari za Punde

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, kushirikiana kwa karibu na Idara ya Utumishi, ili kuajiri waalimu nchini.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akisisitiza jambo alipokuwa akizungumza na Wananchi wa Mwambe Mkoa wa Kusini Pemba wakati wa ufunguzi wa Skuli ya Msingi Mwambe ikiwa ni shamra shamra za Maadhimisho ya   miaka 59 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameigaiza wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, kushirikiana kwa karibu na Idara ya Utumishi, ili kuajiri waalimu nchini.                                                                                                              

Alisema, changamoto ya uhaba wa waalimu anajua kuwa, ipo, lakinini ni vyema kwa wizara husika, kuongeza kasi ya kuajiri waalimu na kipaumbele, iwe ni wale ambao walishajitolea siku za awali.

Alieleza kuwa, wakati serikali ikijenga skuli mpya zikiwemo za ghorofa na kuzifanyia ukarabati zile za zamani, lazima na suala la kuajiri waalimu nalo liangaliwe kwa haraka.

Dk. Mwinyi ameyasema hayo Mwambe wilaya ya Mkoani Pemba, mara baada ya kuifungua skuli mpya ya ghorofa mbili ya msingi Mwambe, wakati akizungumza na wanafunzi na wananchi wengine, ikiwa ni shamra shamra za miaka 59, ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.

Alieleza kuwa, anasisitiza kuwa, wakati wizara hiyo ikiajiri waalmu wakiwemo wa masomo ya sayansi, iwape kipaumbele waalimu wenye sifa, na ambao walishawahi kujitolea, ili kuzingatia moyo wao wa kizalendo waliouonesha.

‘’Kama walionesha moyo wa kujitolea kwa taifa lao, kwa kuwatumikia wananchi wenzao, sasa wakati ukifika wa uajiri, nao wapewe kipaumbele kwa wenye sifa,’’alisisitiza.

Katika hatua nyingine Rais huyo wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameahidi kujenga skuli nyingine ya ghorofa eneo hilo la Mwambe, ili kukabiliana na uwingi wa wanafunzi uliopo.

Alieleza kuwa, ameshtushwa na idadi ya wanafunzi wanaoendelea kuandikishwa wa darasa la kwanza kwa mwaka huu, ambao kwa sasa wameshafikia 970.

‘’Kwa hili, lazima niwaahidi wananchi wa Mwambe na vijiji jirani kuwa, serikali itajengwa tena skuli nyingine ya ghorofa, ili mwakani tukisherehekea miaka 60 ya Mapinduzi, nayo iwepo,’’alieleza.

Hata hivyo rais huyo ameelezeam kuridhishwa na usimamizi mzuri wa fedha wa shilingi bilioni 68, walizopewa wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, kwa ajili ya ujenzi wa skuli mbali mbali nchini.

Hata hivyo alisema, bado serikali ya awamu ya nane, itaendelea kuona kuwa, elimu ndio kipaumbele cha kwanza, na azma ya kujenga skuli za kisasa na vifaa vya kufundishia ipo.

‘’Ndio maana zipo skuli 24 za zamani kwa Unguja na Pemba, zinaendelea kufanyiwa matengenezo makubwa, ambapo kwa wilaya ya Mkoani, ni skuli za Mauwani Kiwani, Chambani na Maendeleao Ngwachani.

Hata hivyo alisema, ndani kipindi cha mwaka mmoja, serikali imeshajenga madarasa 143, kati ya hao 95 yalianzishwa kwa nguvu za wananchi na 48 ndio mapya, samba mba na ujenzi wa vyoo 318 kwa skuli za maandalizi, msingi na sekondari mkoani humo.

Kuhusu mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, alisema kuwa, moja ya shabaha ni kuhakikisha watoto wa taifa hili, wanapata nafasi ya kujifunza, wakiwa kwenye skuli kisasa.

Alisema, ndio maana serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya awamu ya nane, imeweka kipaumbe cha miradi mbali mbali ya wananchi, ikiwemo ya elimu, ili kupunguza athari za ukosefu wa makaazi ya kisasa ya kujifunzia.

‘’Leo tukiwa tunaadhimisha miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar, tunayo mengi ya kujivunia, ikiwa ni pamoja sekta ya elimu, afya, miundombinu ya barabara na huduma nyingine za kijamii, kuimarika,’’alieleza.

Kwa upande wake Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Leila Mohamed Mussa, alisema kasi ya Dk. Mwinyi ndani ya wizara hiyo, imesaidiai kutatua changamoto mbali mbali, zikiwemo za maakazi.

Alisema, sio Mwambe pekee lakini kila wilaya ya Unguja na Pemba, Rais huyo, ameshaacha alama kwa kuhakikisha kunajengwa skuli za kisasa na za ghorofa, kuingiza na fanicha zake kamili.

‘’Malengo ya Mapinduzi ya Zanzibar baada ya kuasisiwa na viongozi waliotangulia, sasa yanaendelezwa kwa kasi na serikali ya awamu ya nane, chini ya Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwa hili hongera sana,’’alisema.

Aidha alimpongeza Dk. Hussein kwa kuwapatia fedha shilingi bilioni 68,kwa ujenzi wa skuli na kutia samani, na ununuzi wa vitabu, sambamba na kukamilisha ujenzi skuli 25 za maandalizi Unguja na Pemba.

Nae Katibu Mkuu wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Khamis Abdalla Said, alisema ujenzi huo ambao sasa umejumuisha madarasa 46, yakiwemo 5 ya zamani

Alisema kuwa, fedha za sherehe ya mapinduzi shilingi milioni 450, zitawasaidia kwa ununuzi wa samani na vitambu katika skuli mbali mbali za Unguja na Pemba.

Alifahamisha kuwa, ujenzi wa skuli hiyo na nyingine ni utekelezaji wa ahadi zake kwa vitendo, alizozitoa kipindi cha kampeni.

‘’Skuli hii yenye ghorofa mbili na moja ya chini (ground) ni ya kwanza kwa Zanzibar, ambayo itapunguza changamoto ya makaazi wa wanafunzi wa Mwambe,’’alieleza.

Hata hivyo aliafafanua kuwa, wizara tayari imeshaingiza viti, meza mpya na za kisasa ndani ya skuli hiyo na iko tayari kwa ajili ya kuhamiwa.

Skuli hiyo ya ghorofa mbili ya msingi ya Mwambe wilaya ya Mkoani Pemba, ujenzi wake umechukua mwaka mmoja, umejengwa na kampuni na Mwamba kwa shilingi bilioni 3.571 fedha za UVIKO 19, kupitia Shirika la Fedha Duniani ‘IFM’.

Imetayarishwa na Idaya ya Mawasiliano

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.