SERIKALI ya Mapinduzi
ya Zanzibar imeitaka kampuni ya kimataifa, Puma Energy kuangalia uwezekano wa
kupunguza bei ya mafuta ya ndege ili kuendana na soko la ushindani la
kimataifa.
Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi wakati akizungumza na
uongozi wa kampuni hiyo, Ikulu Zanzibar amesema ongezeko la bei ya maputa kwa
kampuni hiyo inaiathiri Zanzibar kwa baadhi ya kampuni kubwa za ndege kushindwa
kutua nchini kwa hofu ya kukosa mafuta.
Aliishauri kampuni
hiyo kushusha bei ili kuendana na soko la ushindani hasa kwa kampuni za usafiri
wa anga na wadau wengine kwenye sekta ya usafirishaji.
Alisema kuna mgogoro
mkubwa kwenye sekta hizo uliosababishwa na kupandisha gharama za mafuta ya
ndege, hali inayosababisha baadhi ya kampuni kubwa za ndege kununua Dar es
Salaam na Mombasa, aidha, Dk. Mwinyi alieleza wanaoathirika zaidi ni kampuni
ndogo za ndege zinazofanya safari zake za ndani baina ya Pemba, Tanga na Dar es
Salaam.
Hata hivyo,
aliwashauri Puma Energy kutoridhika na hali hiyo, badala yake wakubaliane na
hali halisi ya soko la ushindani lilivyo ili kutoa fursa ya soko la biashara
kwa kila mwekezaji.
Aliwaeleza kampuni
hiyo endapo watashindwa pungunguza gharama za mafuta na kukabiliana na ushindani
wa kibiashara uliopo kwenye usafirishaji wa anga, Serikali tayari imeiagiza
Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar (ZAA) kuangalia uwezekano wa kampuni
nyengine kupewa fursa ya kuhudumia eneo hilo.
Alidha, alisema
Serikali ina dhamira njema kwa wawekezaji wote pia inaunga mkono jitihada wanazozifanya
kwa Serikali katika kuwahudumia watu na mazingira mazuri ya biashara, hivyo
aliwataka wawekezaji kukabiliana na ushindani kwa kuleta unafuu kwa kila mmoja.
Pia Dk. Mwinyi alieleza
Serikali imedhamiria kufanya uwekezaji mkubwa wa kuhifadhi mafuta ya kutosha
ili kujiweka tayari na tatizo lolote, kupata utatuzi wa haraka.
Aliishauri Kampuni ya
Puma Energy kuangalia fursa za uwekezaji wa eneo hilo kwa bandari ya Mangapwaji
kuweka chemba ya kushushia mafuta na ghala la kuhifadhia mafuta ya ndege.
“Kwa hali tuliyonayo
sasa likitokea tatizo lolole ingawa hatuombi litokee, hatutokuwa na uwezo wa
kulitatua kwa vile hatuna hakiba” alieleza Dk. Mwinyi.
Alisema Serikali
inajipanga kuhifadhi mafuta ya ziada ili iwe na uwezo wa kukabiliana na
changamoto itakayotokea kwa kuziba mianya ya athari za changamoto hizo.
Akizungumzia ujenzi
mpya wa uwanja wa ndege wa Pemba, Rais Dk. Mwinyi alisema Serikali imedhamiria
kuweka uwiano sawa na mandhari ya kisiwa cha Unguja kwa uondoa utofauti wa
maendeleo na uwekezaji baina ya visiwa viwili hivyo.
Alisema tayari kuna
wadau wengi wamejitokeza kuwekeza eneo hilo na kuwaeleza Puma Energy kuangalia
fursa wa uwekezaji kwenye mradi huo.
Naye, Mkurugenzi
Mtendaji wa Puma Energy kanda ya Afrika, Fadi Mitri aliiambia Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar kwamba wana nia njema ya kuwekeza Pemba kwenye uwanja mpya wa ndege
wa kimataifa kuwa wa kisasa na bora zaidi kwa Afrika nzima kuongoza kwa huduma
za kimataifa na vifaa vyenye ubora wa uhakika.
Alisema kamuni ya
Puma Energy itawekeza kwenye miundombinu ya kisasa ya uwanja huo, ipo tayari
kutoa huduma za ndege za kimataifa kwenye uwanja huo kama ilivyo kwa kampuni ya
Dnata ambayo inatoa huduma bora za viwanja vya ndege vya kimataifa kupitia mataifa
mbalimbali ulimwenguni.
Alisema licha ya
Dnata kutoa huduma kwa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Aman Karume,
Kisauni Unguja, alisema kwa kisiwa cha Pemba, kampuni yake ya Puma Energy iko
tayari kuhudumia na wameahidi kwa Serikali kwamba wataungamkono kwenye sekta
hiyo.
Aidha, aliiahidi
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuongeza ndege zaidi za kimataifa kuja moja
kwa moja Zanzibar, alisema Puma Energy wanahudumia ndege zaidi ya 80 nchini
Afrika Kusini. Hivyo, uwezo wa kuongeza ndege kufanya safari zake Zanzibar ni
rahisi sana kwao.
Alisema
watashirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuifanya Zanzibar kuwa
kituo bora zaidi kwa wageni kufikia na rahisi kufikiwa kwa kufurahia uzuri wa
mandhari na haiba ya visiwa vyake.
Kampuni ya Puma
Energy yenye makao makuu yake nchini Singapore, inafanyakazi kwenye viwanja vya
ndege zaidi ya 80 duniani kote pia ina vituo 740 kwa nchi 50 za Afrika, ni
sehemu ya kampuni kubwa duniani ya Trafigura ambayo inafanyakazi kwa zaidi ya
nchi 40 kutoka mabara Matano ya dunia.
IDARA YA MAWASILINO, IKULU ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment