Habari za Punde

Chama Cha Mapinduzi (CCM ) Zanzibar Yampongeza Mhe.Dk.Mwinyi kwa Kutunukiwa TUZO

Na.Is-haka Omar - Zanzibar.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, kimempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwa kutunukiwa Tuzo Maalum ya VIP Global Water Changemakers Awards kutokana na jitihada zake za kuifanya Zanzibar kuwa nchi ya kwanza Barani Afrika kuanzisha na kuzindua program ya uwekezaji katika sekta ya maji.

Akitoa pongezi hizo Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idarea ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar  Khamis Mbeto Khamis, amesema tuzo hiyo imetokana na juhudi za kuwatumikia wananchi katika kumaliza tatizo la upungufu wa maji safi na salama nchini zinazofanywa na  Rais wa Zanzibar Dk.Mwinyi.

Mbeto, alieleza kuwa Tuzo hiyo imetolewa pembezoni mwa Mkutano wa Maji wa Umoja wa Mataifa tarehe: 22 Machi, 2023 jijini New York ina lengo la kutambua na kuthamini mchango wa viongozi katika uwekezaji wa sekta ya maji kwenye nchi zao.

Alisema kwa mujibu wa Taarifa kutoka Idara ya Mawasiliano ya Rais Ikulu ya Zanzibar imefafanua kuwa Rais wa Zanzibar Dk.Mwinyi, amewakilishwa kupokea Tuzo hiyo na Balozi Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania Umoja wa Mataifa Dkt. Suleiman H. Suleiman Jijini New York.

Katika maelezo yake Mbeto, alisema kupitia heshima hiyo CCM ina imani kuwa Rais Dk.Mwinyi, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, ataendelea kufanya juhudi kubwa za kumaliza tatizo la ukosefu wa maji nchini pamoja na changamoto nyingine  ili wananchi wapate huduma hiyo kwa wakati.

Alieleza kuwa katika kipindi cha miaka mitano (2020-2025) Chama Cha Mapinduzi kiliahidi kupitia ilani yake ya Uchaguzi ukurasa wa 243 ibara ya 186 vifungu vidogo vya (a)-(i) kuwa katika miaka mitano ijayo,CCM inaielekeza SMZ kuendelea kutimiza azma ya ASP na CCM ya kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wote katika maeneo ya mijini na vijijini.

Alieleza kwamba dhamira ya CCM ni kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma ya uhakika ya maji safi na salama bila vikwazo kwani nishati hiyo ndio kipaumbele cha maisha ya kila siku ya mwanadamu kutokana na umuhimu wake katika matumizi ya kila siku.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.