

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii ikiongozwa na Mwenyekiti Mhe. Timotheo Mnzava (Mb) katika picha ya pamoja ilipotembelea Mamlaka ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kwa ajili ya kukagua mradi wa ujenzi wa Barabara ya Seneto hadi Kreta Mkoani Arusha.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeridhishwa na teknolojia ya tabaka gumu la mawe iliyotumika katika ujenzi wa Barabara ya Seneto hadi Kreta katika Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro.
Mwenyekiti wa Kamati ya
Kudumu ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhe. Timotheo Mnzava(Mb) ametoa kauli
hiyo leo wakati wa ziara ya kukagua mradi wa ujenzi wa barabara katika Mamlaka
ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro Mkoani Arusha
“Kwa kweli tumefurahishwa
sana na aina hii ya teknolojia iliyotumika katika ujenzi wa barabara na sisi
kama Kamati tutaendelea kuishauri Serikali kuitumia katika maeneo mengine
yanayohitaji teknolojia ya aina hii” Mhe. Mnzava amesisitiza.
Amefafanua kuwa awali
barabara hiyo ilikua changamoto kwa watalii wanaoingia katika eneo la Kreta
lakini kwa kazi iliyofanyika itaendelea kuwavutia wageni na kuhakikisha usalama
wa wageni wanaotembelea Kreta ya Ngorongoro.
Mhe. Mnzava ameipongeza
Serikali kwa kutoa fedha zilizotumika katika ujenzi wa barabara hiyo na pia
ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la
Ngorongoro kwa kuisimamia kazi ya ujenzi.
Ametoa wito kwa Serikali
kuongeza juhudi na kasi katika kumalizia kipande cha barabara kilichobakia
lakini pia kuangalia uwezekano wa kukarabati barabara nyingine za Ngorongoro
ili kukuza utalii na kuongeza usalama wa watalii wanaotembelea eneo hilo.
Naye, Naibu Waziri wa
Maliasili nanUtalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amesema barabara hiyo ni hazina
katika hifadhi kwa sababu imejengwa kwa kuokoa gharama ambapo awali zilipangwa
kutumika kiasi cha shilingi bilioni 1.9 lakini imetumia kiasi cha shilingi
bilioni 1.7.
Amesema mfumo wa barabara za
mawe ni bora zaidi kwa sababu ni rafiki wa uhifadhi na gharama nafuu
ukilinganisha na barabara za lami.
Ameongeza kuwa maelekezo yote
ya Kamati ya kumalizia eneo la barabara lenye urefu wa kilomita 1.2 na
kuangalia uwezekano wa kutumia teknolojia ya mawe katika maeneo mengine
uhifadhi yatafanyiwa kazi.
Ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara katika uhifadhi na uendelezaji wa utalii ambapo moja ya mikakati yake ni kuhakikisha miundombinu katika maeneo yote yaliyohifadhiwa iwe rafiki kwa watalii ili iwezeshe kuongeza idadi ya watalii.
No comments:
Post a Comment