MASHIRIKA ya
Umma yametakiwa kujitathmini kwa kujipambanua na kufungua ukurasa mpya wa
ufanisi na uendeshaji kwa kuacha utendaji wa kusuasua badala yake kuja na
mikakati ya mageuzi na kuleta mabadiliko ya haraka yenye kutoa huduma za
uhakika kwa wananchi na tija kwa Serikali.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Hussein Ali Mwinyi, aliyasema hayo Ikulu Zanzibar, alipozungumza na Watendaji
wakuu wa mashirika hayo na kuwaelekeza kufanya marekebisho na maboresho ya
kiutendaji watakapoona mazingira hayapo sawa kwa mustakbali wa mashirika hayo
na Serikali kwa ujumla.
“Tunataka mashirika ya umma
yaendane na kasi ya awamu ya nane kwa kufungua ukurasa mpya wa nidhamu, ukurasa
wa kufanya kazi kwa bidii, ukurasa wakuleta faida na kubwa kuliko lote ni
huduma za uhakika kwa wananchi, wanachotaka kutoka kwetu Serikali ni huduma za
uhakika, haitoshi kutetea tuu maji na umeme iwe uhakika” aliasa Dk. Mwinyi.
Dk. Mwinyi ameyataka mashirika yanayotoa huduma kwa wananchi
kutafuta ufumbuzi wa haraka kutatua changamoto zinazowakabili na kuzigeuza kuwa
fursa zenye tija kuleta mabadiliko chanya ikiwemo kubadili mifumo ya taasisi
zao inapoonekana inafaa kwa maslahi ya umma.
Akiizungumzia Mamlaka ya Maji Zanzibar, (ZAWA) na Shirika la
Umeme Zanzibar (ZECO) Rais Dk. Mwinyi alieleza ni Mashirika yanayotoa huduma na
kugusa maisha ya watu moja kwa moja na kueleza haitoshi kutoa huduma pekee bila
ya kuingiza faida kwa ajili ya uendeshaji wa mashirika hayo.
Aliwaelekeza watendaji wa mashirika hayo wajitathmini na
huduma wanazowapatia wananchi na kwa nini wakose faida aidha, aliyataka
mashirika hayo kubadilika na kuwapatia wananchi huduma za uhakika kwa kuongeza
kasi ya utendaji wao na wajiendeshe kwa mikakati ya uwekezaji ili wajiepushe na
hasara na huduma zisizokidhi haja za wananchi. Hata hivyo, aliwashauri kuja na
mpango wa utekelezaji kwa kuangalia upya vyanzo vya matatizo waliyonayo na
kuyatafutia ufumbuzi wa haraka.
Aidha, aliwashauri ZAWA kuacha kutumia pampu zinazotumia
umeme wa ZECO badala yake watumie za umeme wa jua ama solar ili kukwepa
matatizo ya kuungua kila mara na kuwaondolea wananchi shida ya kukosa maji mara
kwa mara.
Kwa Mashirika yanayojitegemea, Rais Dk. Mwinyi aliyashauri
kutafuta mitaji kujiwekeza kwenye uzalishaji wenye faida kwa mustakabali wa
Mashirika hayo na Serikali kwa ujumla.
Kwa Mashirika yanayojitegemea,
Rais Dk. Mwinyi aliyashauri kutafuta mitaji kuwekeza kwenye uzalishaji wenye
faida kwa mustakabali wa Mashirika hayo na Serikali kwa ujumla.
Akizungumzia baadhi ya Mashirika
ya Umma yanayosuasua kwenye uzalishaji, Rais Dk. Mwinyi aliwaeleza uwekezaji
zaidi unahitajika ili yajiendeshe kibiashara na kuongeza Serikali inahitaji uwekezaji
mkubwa kwa baadhi yao ili kuwapa nafasi ya kufanya vizuri.
“Ukipewa taasisi ukiona mambo
hayapo sawa badilisha na kuweka ufanisi wenye tija kwa Serikali na maslahi kwa
wananchi kama huna uwezo rudi tukusaidie” Alishauri Dk. Mwinyi.
Alisema hakuna sababu ya mashirika
ya Umma kupata hasara, alieleza kuna mambo kama Serikali imeshindwa hayafanya
hakuna sababu ya kuendelea kupata hasara badala yake alishauri kupewa Sekta
binafsi kufanya ili serikali ipate faida na wananchi wapate huduma
wanazostahiki kwa wakati unaofaa, akitolea mfano Mamlaka ya Viwanja vya ndege
Zanzibar (ZAA). Alisema awali taasisi hiyo ilikuwa inapata
hasara hadi serikali ilikua ikitoa fedha zaA mishahara lakini baada ya taasisi
hiyo kushirikiana na sekta binafsi imekua ikiingiza faida kubwa.
Akiyazungumzia mashirika ya umma
yanayojiendesha yenyewe kama Shirika la Bima, ZMUX na mashirika mengine, Rais Dk.
Mwinyi aliyashauri kutafuta mitaji na kujiendesha kibiashara hususan ZMUX ili
kuendana na soko la ushindani.
Kuhusu Shirika la nyumba, Dk.
Mwinyi alilielezea shirika hilo kwamba halina kasi ya kujiendesha kwa kukosa
mtaji wa kukarabati na kufanya matengenezo ya nyumba tokea zilipojengwa mwaka
1972 hadi sasa.
“Mkisema mna nyumba Michenzani
sio nyumba tena, Kilimani hamna nyumba, kikwajuni zote zinahitaji ukarabati na
kujengwa upya, ifike sehemu shirika hili liweze kukarabati, kujenga nyumba mpya
na kufanyakazi kibiashara” alishauri Dk. Mwinyi
Pia Rais Mwinyi alilishauri
Shirika hilo kuja na mpango utakaoonesha mahitaji ya matengenezo na maboresho
ya nyumba hizo ama kujenga mpya na kuonesha marejesho ya uwekezaji ili nyumba
hizo zileendelee kuleta tija kwa wananchi na Serikali.
Rais Dk. Mwinyi aliligeukia
Shirika la Biashara la ZSTC na kulitaka kubuni mbinu endelevu za uzalishaji kwa
kuhakikisha wananunua karafuu zilizosafishwa ili kukwepa hasara kwa serikali.
IDARA YA
MAWASILIANO
IKULU, ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment