Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Mwinyi Amezungumza na Uongozi wa ZABESA

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi,alipokuwa akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo na Uongozi wa Chama cha mazoezi ya Viungo   Zanzibar (ZABESA) ulioongozwa na Mwenyekiti Ndg,Said Suleiman Said (wa tatu kushoto)  wakati Uongozi  huo ulipofika Ikuu Jijini Zanzibar leo. 02/03/2023.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akipokea taarifa ya Chama cha Mchezo wa mazoezi ya Viungo Zanzibar (ZABESA) kutoka kwa Mwenyekiti  Ndg.Said Suleiman Said wakati Uongozi wa Chama hicho ulipofika Ikuu Jijini Zanzibar leo
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi,alipokuwa akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo na Uongozi wa Chama cha mazoezi ya Viungo   Zanzibar (ZABESA) ulioongozwa na Mwenyekiti Ndg,Said Suleiman Said (hawapo pichani) wakati Uongozi  huo ulipofika Ikuu Jijini Zanzibar leo.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amevipongeza vikundi vya vya mazoezi ya viungo kwa kuimarisha afya zao na kuwaweka watu pamoja hatua aliyoieleza inaisaidia Serikali kupunguza magojwa yasiyoambukiza kwa kujenga taifa imara lenye nguvu kazi.

Dk. Mwinyi alitoa pongezi hizo, IKulu, Zanzibar alipozungumza na uongozi wa chama cha wafanyamazoezi ya viungo, Zanzibar (ZABESA).

Alisema hamasa inayotolewa na vikundi hivyo, ni njia sahihi ya kupambana na magonjwa hayo yakiwemo presha, kisukari na matatizo ya moyo ambayo Dk. Mwinyi alieleza magonjwa hayo yanaigharimu sana Serikali na kupunguzu nguvu kazi.

“Nawapongeza sababu jambo mnalolifanya lina tija na kuimarisha afya za watu, Serikali inathamini sana juhudi yenu hii na tunakupeni moyo muendelee kuwashajihisha waliokuwepo wasitoke na wasiokuwepo wajiunge kwani kinga ni bora kuliko tiba” alisifu Dk. Mwinyi.

Alisema ZABESA mbali yakuwakusanya watu pamoja kuimarisha afya zao pia wanaisaidia Serikali kuifikia jamii kubwa kwa wakati hata ikiamua kutoa msaada ni rahisi sababu watu wako pamoja wenye uongozi mazubuti.

Alieleza vikundi hivyo vimekuwa na tija kwa jamii na kwamba Serikali inawaungamkono na kuwapongeza kwa utaratibu hasa kwa utaratibu wao waliojiwekea kwa kufanya usafi wa mazingira katika maeneo mbalimabli ya Zanzibar ikiwemo kisiwa cha Changuu kwa Unguja na Misali Pemba.

Aidha, Dk. Mwinyi aliwashauri wanamazoezi hao kushirikiana na sekta binafsi zikiwemo bank, kampuni za simu na taasisi nyengine kujitingaza kupitia vikundi hivyo ili kuwasaidia kiuendeshaji na kuviwezesha vikundi hivyo kwa shughuli za ujasiriamali.

“Hatuwezi kuajiri watu wasiohitajika au nafasi zisizokuwepo, kwa hiyo mara zote tumekuwa tukiwashajihisha watu kujiunga kwenye vikundi, ili kuisaidia Serikali hata tukiamua kutoa msaada inakua rahisi kuwasaidia.” Alisema Dk. Mwinyi

Alieleza, hatua hiyo inaisaidia serikali kutekeleza kwa vitendo Ilani ya uchaguzi inayotaka kuwasaidia watu na kutimiza ahadi ya ajira laki tatu na kuongeza kwa vile fursa ya kuajiri serikalini nafasi chache, Serikali inaelekeza nguvu zake kwa vikundi vyenye tija vilivyojikusanya pamoja kwa lengo la kujiletea maendeleo kwa kuviunga mkono kiuchumi.

“Kwa upande wenu wajasiriamali, Serikali inawajibu wa kukusaidieni kuwapa elimu na kukusaidieni kupata mitaji kwa njia ya mikopo, nitaielekeza taasisi ya uwezeshaji wananchi kiuchumi, wakuchukulieni nyinyi kama makundi katika jamii ili mkiendana na sifa zao wakupeni elimu na mikopo inayaotakiwa” Dk. Mwinyi aliiahidi ZABESA.

Pia, Dk.Mwinyi aliwaahidi kushirikiana nao  kutafuta waatalamu wa Mazoezi  watakaojitolea kufundisha vikundi hivyo na kuendeleza mazoezi nchini. 

Naye, Mwenyekiti wa ZABESA, Said Suleiman Said na timu aliyoongozanayo walimpongeza Rais Dk.Mwinyi kwa kutimiza miaka miwili ya Uongozi wake wa kuwatumikia Wazanzibari katika kuwaletea maendeleo makubwa sambamba na kuchaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, Zanzibar. 

Walieleza ZABESA imebadili mtazamo wa jamii kuamini vikundi hivyo kwaajili ya mazoezi pakee bali wameelekeza fikra zao kwenye masuala ya ujasiriamali na uzalishaji ili kujiajiri kwa vijana, wazee wasio na ajira rasmi kwa lengo la kujikwamua kiuchumi mara baada ya mazoezi pamoja na kusafisha mazingira kwenye miji ili kuvutia watalii.

Aidha, waliishukuru Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale kwa kuungamkono juhudi za chama hicho hasa kwenye juhudi za utunzaji mazingira kwenye maeneo ya utalii na kuahidi kwamba ZABESA itayafikia maeneo mengi kwa usafi ikiwemo sekta ya Afya.

Mwenyekiti Said alieleza mbali na malengo iliyojipangia ZABESA impango wa kuungana na dunia kuadhimisha siku ya usafi ulimwenguni kote ambayo huadhimishwa kila Jumamosi ya tatu ya mwezi wa Septemba kwa kila mwaka, hivyo walitumia fursa hiyo kumuomba Rais Dk. Mwinyi kuizindua rasmi siku hiyo kwa Zanzibar ili kungana na jamii ya kimataifa katika kuimarisha mazoezi ya viungo. 

IDARA YA MAWASILIANO

IKULU, ZANZIBAR. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.