Habari za Punde

Tanzania Yaungana na Nchi Nyengine Duniani Kuadhimisha Siku ya Kupinga Unyanyapaa na Ubaguzi Nchini

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe.Rosemary Senyamule,akizungumza leo Machi 1,2023 jijini Dodoma wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Unyapaa na Ubaguzi yanayofanyika Machi Mosi kila Mwaka.
Baadhiya ya Washiriki wakifatilia hotuba ya Mkuu  wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule (hayupo pichani) wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Unyapaa na Ubaguzi yanayofanyika Machi Mosi kila Mwaka yaliyofanyika leo Machi 1,2023 jijini Dodoma.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe.Rosemary Senyamule,akiwa katika picha ya pamoja na Watendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) mara baada ya kuzungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Unyapaa na Ubaguzi yanayofanyika Machi Mosi kila Mwaka yaliyofanyika leo Machi 1,2023 jijini Dodoma.

(Picha Zote na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Na. Mwandishi wetu- Dodoma

TANZANIA imeungana na nchi nyingine Duniani kuadhimisha Siku ya Kupinga Unyanyapaa na Ubaguzi Duniani inayoadhimishwa kimataifa Machi Mosi kila mwaka ili kuendelea kupaza sauti juu ya kupinga na kupiga marufuku vitendo vyote vya unyanyapaa.

Madhimisho hayo yamefanyika Machi 1, 2023 Jijini Dodoma ambapo Mgeni Rasmi alikuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe.George Simbachawene.

"Kauli mbiu ya mwaka huu ni TOKOMEZA UBAGUZI, OKOA MAISHA inaonyesha namna  ubaguzi na kukosekana kwa Usawa na Haki ni miongoni mwa changamoto zinazosababisha vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia na ukatili,"Alisema Mhe. Senyamule.

Alieleza kuwa  Dhana na vitendo vya Ubaguzi vinavyoashiria Ukatili na kutokuwepo kwa usawa vinasababisha kutotimia kwa Malengo  ya Kitaifa ya mwitikio wa VVU na UKIMWI na kurudisha nyuma jitihada za Serikali za kutokomeza UKIMWI.

Akifafanua kuhusu kauli mbiu ya mwaka huu, alisema kuwa inatutaka kuangalia umuhimu wa kuhakikisha tunatokomeza ubaguzi na unyanyapaa miongoni mwa watu wanaoishi na VVU na makundi mengine.

Katika hatua nyingine amebainisha viashiria ambavyo huchangia kuongezeka kwa maambukizi mapya ikiwemo; mila potofu, ubaguzi, kutengwa na unyanyapaa kwa namna mbalimbali.

Ameeleza kuwa kwa mujibu wa Takwimu zinaonesha wanawake na wasichana ndiyo makundi yanayoathiriwa zaidi na vitendo vya unyanyapa na ubaguzi katika jamii.

“Baadhi ya wanawake na wasichana wamepata maambukizi ya VVU kutokana na ukatili wa kingono, Wanawake wenye VVU wapo katika hatari ya ukatili hasa baada ya kuweka wazi hali zao za maambukizi,”alisisitiza Mhe. Senyamule.

Vile vile, amesema uwepo wa ubaguzi katika maeneo muhimu ikiwemo ya ya utoaji wa maamuzi kwa kundi la wanawake limeendelea kuachwa nyuma hivyo kusababisha kukosekana kwa usawa wa kijinsia.

Hata hivyo amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Baraza la NACOPHA wameweza kufanikisha kuhamasisha watu wanaoishi na VVU kujiunga katika Konga ambapo hushirikiana pamoja kujikwamua kiuchumi, kupeana taarifa mbalimbali, na hata kuhudumiana.

“Nachukua fursa hii kuwapongeza wadau wote na mashirika yanayotoa msaada kwa watu wanaoishi na VVU na watoto yatima. Aidha nawapongeza TACAIDS na Baraza la watu wanaoishi na VVU kwa kuendelea kusimamia maslahi pamoja na haki za ustawi wa watu wanaoishi na VVU nchini”Alisema

Pia amesema Serikali imehakikisha Dawa za ARV zinaendelea kupatikana nchini bila kikwazo chochote, hivyo wale wote wanaogundulika kuwa na VVU waanze na waendelee kutumia ARV kama inavyooelekezwa na wataalamu wa Afya.

Serikali ya Tanzania imeweka sera na mifumo mizuri ya kisheria, mipango ya kitaasisi na miongozo ya kitaifa ambayo imetengeneza mazingira mazuri ya kuboresha haki za binadamu, usawa wa kijinsia pamoja na ushirikiano wa jamii.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa NACOPHA Bw. Yusuph Marere, amesema Katika maadhimisho hayo wanaungana na wenzao Duniani kote kuhakikisha kuwa kila mmoja anaishi kwa kuzingatia heshima na utu wa binadamu bila ubaguzi wa aina yoyote.

“Siku hii muhimu inatukumbusha kuwa kila mmoja anapaswa kuheshimu na kuheshimiwa na vilevile inatukumbusha kuwa na mifumo, sera na huduma jumuishi zinazohusisha makundi yote katika jamii na pia tunakumbushwa kupinga aina zote za unyanyapaa na ubaguzi kwa WAVIU na watu walio katika makundi maalumu”,amesema Bw.Marere

Ameeleza kuwa kwa kiasi kikubwa unyanyapaa na ubaguzi katika jamii umechangia watu wengi kushindwa kujitokeza ili kupata huduma bora za VVU na UKIMWI ikiwemo upimaji wa hiari, tiba na matunzo.

“Juhudi za dhati zinahitajika ili kukomesha hali hii katika Taifa letu na kwa kufanya hivyo tunaweza kufikia malengo ya Dunia ya kutokomeza UKIMWI ifikapo 2030,”alisema.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.