Habari za Punde

CCM Zanzibar Yatekeleza Ahadi yake Kijiji cha Kangagani Pemba

KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Ndugu Khamis Mbeto Khamis,akikabidhi mashine ya maji safi na salama kwa mwananchi wa kijiji cha Kangagani Pemba ndugu Suleiman Ali Suleiman, iliyotolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt.Mohammed Said Mohammed ‘Dimwa’.
BAADHI ya wananchi wakiwa katika futari hiyo iliyoandaliwa na Makamu wa Pili wa rais wa Zanzibar Hemed Suleiman uko Tibirinzi Pemba.

NA IS-HAKA OMAR, PEMBA.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar,kimesema kitaendeleza utamaduni wake wa kutekeleza ahadi zake kwa vitendo kwa nia ya kumaliza changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.

Hayo ameyasema Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi Khamis Mbeto Khamis,wakati akikabidhi mashine ya maji safi na salama kwa mwananchi wa kijiji cha Kangagani Wilaya ya Wete Pemba ndugu Suleiman Ali Suleiman.

Alisema dhamira ya Chama Cha Mapinduzi ni  kuendelea usimamia kikamilifu utekelezaji wa ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2020/2025 kwa kuhakikisha changamoto ya tatizo la ukosefu wa maji safi na salama inamaliza nchini.

Katibu huyo Mbeto, alisema mashine hiyo ya maji imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Dkt.Mohammed Said Mohammed, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yake aliyotoa hivi karibuni aliposhiriki katika dua maalum ya kuiombea amani nchi.

Katika maelezo yake Katibu huyo wa NEC Mbeto, alisema maji safi ni nishati muhimu katika maisha ya kila siku ya mwanadamu hivyo serikali kupitia taasisi zake zinazosimamia upatikanaji wa huduma hiyo ziongeze juhudi za kutatua changamoto hiyo.

“ Chama Cha Mapinduzi Afisi Kuu ya Zanzibar leo tunakabidhi mashine hii ya maji safi na salama ili kuwaondolea usumbufu wa ukosefu wa maji katika kijiji hiki.

Pia Naibu Katibu mkuu Dkt.Dimwa,kanielekeza niwambie kuwa muendelee kukiamini Chama na Serikali zake mbili huku mkidumisha amani,upendo na mshikamano.”, Alitoa salamu hizo Mbeto kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar.

Pamoja na hayo mapema Katibu huyo alishiriki katika hafla ya Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Mhe.Hemed Suleiman Abdulla aliyekabidhi futari kwa watumishi wa CCM wa Mkoa wa Kusini Pemba.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi futari hiyo  Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman, alisema ametoa sadaka hiyo kwa watumishi hao wa Chama na ataendelea kutoa kwa mikoa mingine ili wapate futari ya uhakika katika mwezi huu wa Ramadhani.

“Nipo katika ziara yangu ya kiserikali ya kutembelea maeneio mbalimbali na kujumuika na  waumini na wananchi wenzangu wa Pemba, lakini nikaona kuna umuhimu wa kutoa sadaka ndogo kwa watumishi wa CCM wa mkoa huu ambao ni 47 ambapo kila mtumishi atapata kilo 25 ili ziwasaidie katika kipindi hiki cha mwezi wa Ramadhani.”, alisema Mhe.Hemed.

Akitoa shukrani  Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Kusini Pemba  Ndg.Yussuf Ali Juma, amemshukuru Mhe. Hemed kwa uamuzi  wake wa kuwasaidia watendaji wa CCM katika mkoa huo na kwamba hatua hiyo itaongeza ari ya juhudi za kufanya kazi kwa ufanisi.

Aidha, Katibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Ndugu Khamis Mbeto, alishiriki katika hafla ya futari iliyoandaliwa  na Makamu wa Pili wa Rais kwa Mikoa miwili ya Pemba huo katika Viwanja vya ZSSF Tibirinzi Pemba.

Akizungumza kwa niaba ya Makamu wa pili wa Rais, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mhe.Mattar Zahor Masoud,aliwasihi wananchi wa Pemba kuendeleza utamaduni wa kufanya ibada kwa wingi na kuepuka mambo yote yanayoweza kuharibu funga zao.

Pamoja na hayo aliendelea kuwakumbusha wafanyabiashara wa kisiwani humo kuwa wakarimu na wenye imani wakati  wa kuuza bidhaa zao ili kila mwananchi apate fursa ya kumudu kutokana na kipato chake.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.