Habari za Punde

Muungano wa Tanzania ni mfano wa kuigwa na mataifa mengine barani Afrika - Dk.Mwinyi

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akihutubia na kulifungua Kongamano la Kuadhimidha Miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar lililofanyika katika ukumbi wa Sheikh.Idrissa Abdulwakil Kikwajuni Wilaya ya Mjini Unguja Jijini Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Amani iliopo nchini ni hazina na faida kubwa inayojivunia Tanzania ndani ya miaka 59 ya Muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar.

Amesema Muungano wa Tanzania ni mfano wa kuigwa na mataifa mengine barani Afrika yanayopitia wakati mgumu baada ya kupoteza amani ya mataifa yao hali inayodumaza maendeleo kwa nchi hizo na kueleza amani iliopo nchini ni chachu ya mafanikio makubwa na maendeleo yaliyofikiwa Tanzania.

“Amani ukishaizoea huoni thamani yake, mpaka ipotee ndio utaona umuhimu wake, hatuna haja ya kuonja upotevu wa amani yetu, waswahili husema, Sumu haionjwi, tuangalie wenzetu, Wasomali, Wakongo, Walibya kote huko hakuna amani hakuna maendeleo ni vita tu” Aliasa Rais Dk. Mwinyi.

Dk. Mwinyi aliyasema hayo kwenye Kongamano la Miaka 59 ya Muungano wa Tanzania lililofanyika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul Wakili, Kikwajuni wilaya ya Mjini.

Alisema, Tanzania pia inajivunia uhusiano wa dhati na wa damu kwa watu wa pande mbili za Muungano waliojengwa kiimani kujali utaifa wao unaozungumza lugha moja, silka, mila na utamaduni mmoja kutoka kwa waasisi, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Marehemu, Mzee Abeid Aman Karume.

Alisema uhusiano wa Watanzania asilimia kubwa umejengwa na  watu  waliochanganya  damu kwa pande zote za Muungano ambao wamejikuta na uhusuiano wa undugu, hali aliyoieleza ngumu kwao kuitenganisha.

Akizungumzia fursa na faida kadhaa zinazotokana na Muungano wa Tanzania, Rais Dk. Mwinyi alisema raia wa pande mbili za Muungano wanafursa sawa kisiasa, kiuchumi na kijamii na Mtanzania kutoka upande wowote wa Muungano anayohaki ya kugombea nafasi yoyote ya siasa bila vikwazo vyovyote akijitolea mfano yeye aliwahi kuwa Mbunge kwa vipindi vitatu akitokea Zanzibar pia aligombea Ubunge Jimbo la Mkuranga Tanzania Bara na alishinda bila ya kikwazo chochote cha asili yake.

Rais Dk. Mwinyi, aliwaomba  Watanzania kuzitumia vema fursa zinazopatikana kwenye Muungano, ili kuendelea kujiimarisha kiuchumi na ustawi wa maendelo, umoja, amani na mshikamano.

Naye, mtoa mada wa kwanza iliyohusu faida ya Muungano Afrika,  Mtaalamu wa Sheria na mwanaharakati kutoka Kenya, Prof. Patrick Lumumba, alikieleza kizazi cha sasa cha Tanzania kina jukumu la kujikomboa kutoka kwenye minyororo ya uchumi ya wakoloni mamboleo na kuwaasa wajiepushe na siasa chafu, ukabila, dini na wendelee kuwa wazalendo wa taifa lao na kuweka mbele maslahi ya taifa.

Naye, Mwanasiasa Mkongwe na Waziri mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mzee Steven Wasira akiwasilisha mada ya “Historia na umuhimu wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar”, aliwaasa vijana na Watanzania kwa ujumla kufuata maelekezo na maono ya viongozi wao ili kuimarisha amani iliyopo, umoja na mshikamano baina yao kwa lengo la kukuza maendeleo ya taifa.

“Watanzania tuna bahati kubwa ya kuwa na viongozi wenye maono na uelewa mpana juu ya Muungano wetu huu, Mhe Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania aliwahi kuwa Waziri kwenye Seriali ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, akawa waziri wa Muungano, pia aliwahi kuwa Makamo wa Rais na Rais Dk. Hussein Mwinyi  pia aliwahi kuwa Waziri wa Ulinzi kwa muda mrefu, hivyo Muungano wa Tanzania anaujua sana”. Alieleza.

Akizungumzia mada iliyohusu “Fursa zilizopo kwa vijana ndani ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Balozi Mohamed Hamza alisema Watanzania wa pande zote mbili za Muungano wanafursa sawa ikiwemo ajira kwa sekta za Muungano, zikiwemo nafasi za uongozi, uwakilishi wa kimataifa, mikopo sawa kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu, muhimu wawe na vigezo kwenye fursa hizo ikiwemo uwezo na sifa bila ubaguzi wowote.

IDARA YA MAWASILIANO IKULU, ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.