Habari za Punde

Shirika la Bima la China (SINOSURE) Laahidi Kuendeleza Ushirikiano na Tanzania

Jopo la wataalumu kutoka Wizara ya Fedha na Mipango (kushoto) wakiongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (katikati) wakiwa katika Mkutano na ujumbe wa Shirika la Bima la China (SINOSURE) (kushoto) kuhusu kuongeza ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na China, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dar es Salaam.

Na. Joseph Mahumi, WFM, Dar es Salaam

Shirika la Bima la China - (CHINA EXPORT AND CREDIT INSURANCE CORPORATION (SINOSURE), imeahidi kuendelea kudumisha ushirikiano na Tanzania ambao umekuwepo kwa muda mrefu kwa ajili ya kukuza uchumi na maendeleo ya watu.

 

Ahadi hiyo Imetolewa na Makamu wa Rais wa Shirika hilo Bw. Zha Weimin alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) katika Ofisi Ndogo za Wizara hiyo, jijini Dar es Salaam.

 

Bw. Weimin alisema SINOSURE inafanya juhudi kuwezesha ushirikiano kati ya Tanzania na China kuwa wenye matokeo chanya kwa kushawishi kampuni nyingi za China kuwekeza katika miradi mbalimbali na kufanya biashara Tanzania.

 

“Wafanyabiashara wengi wa China wanawiwa kufanya biashara na Tanzania hivyo jitihada mbalimbali vinazofanyika katika kupunguza vikwazo vya kibiashara na kurekebisha sera katika ushirikiano wetu zitasaidia kuboresha zaidi uhusiano wa kibiashara kati ya nchi hizi mbili” Alisema Bw. Weimin

 

Kwa Upande wake Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amewahikikishia kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kujizatiti kufanya kazi na kushirikiana na Serikali ya China ili kuboresha ushirikiano wa nchi hizo mbili ambao umekuwepo kwa muda mrefu ili kuleta maendeleo ya wananchi. 

 

Dkt. Nchemba alisema kuwa Tanzania inatekeleza ujenzi wa mradi wa kimkakati wa Reli ya kisasa-SGR ambao utaunganisha Tanzania na nchi jirani na ameliomba Shirika hilo kusaidia utekelezaji wa mradi huo Lot 5 kutoka Isaka hadi Mwanza (Km 341) na Lot 6 kutoka Tabora hadi Kigoma ambayo ni takriban Km 506, zote zinatengenezwa na Kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) na China Railway Construction Company (CRCC).

 

“Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania napenda kutoa shukurani zangu za dhati kwa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa msaada mkubwa kwa sekta mbalimbali za uchumi wetu ikijumuisha Miundombinu ya Reli, Elimu, TEHAMA, Nishati, Maji, Usalama, Viwanda na Sekta za Afya. Ni matumaini yetu kuwa ushirikiano huu wa pamoja utaendelea kuimarika zaidi” alisema Dkt. Nchemba.

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (Kulia) akizungumza na Makamu wa Rais wa Shirika la Bima la China (SINOSURE) Bw. Zha Weimin walipokutana na kujadili namna ya kuongeza ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na China, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dar es Salaam.
Makamu wa Rais wa Shirika la Bima la China (SINOSURE) Bw. Zha Weimin (kushoto) akifafanua jambo wakati alipoongoza ujumbe wa Shirika lake walipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb,) (hayumo pichani) wakati wa mkutano kuhusu kuongeza ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na China, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (Kulia) akizungumza jambo wakati wa mkutano na ujumbe wa Shirika la Bima la China (SINOSURE) kuhusu kuongeza ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na China, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (katikati), Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Natu El-Maamry Mwamba (wakwanza kushoto), Kamishna Idara ya Usimamizi wa Deni la Taifa, Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Japhet Justin (wa kwanza kulia) wakiwa katika picha ya Pamoja na ujumbe wa Shirika la Bima la China (SINOSURE) ukiongozwa na Makamu wa Rais wa Shirika hilo Bw. Zha Weimin, baada ya mkutano wao uliofanyika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dar es Salaam.

Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini - (Wizara ya Fedha na Mipango)

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.