SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema itaendelea
kutoa ushirikiano kwa taasisi mbalimbali zinazowahudumia mahujaji wanaokwenda
Makka, Saudi Arabia kutekeleza ibada ya hijja, baada ya kukamika kwa Mwezi
Mtukufu wa Ramadhan.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Al hajj Dk. Hussein Ali Mwinyi, aliyasema hayo alipohutubia Baraza
la Eid -El- Fitri kwenye ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul Wakil, Kikwajuni Mkoa
wa Mjini Magharibi.
Alisema Serikali kupitia kamisheni ya Wakhfu na Mali ya Amana itaendelea kufanyakazi kwa
ushirikino na taasisi hizo ili kuzifanyiakazi changamoto zinazowasababishia
usumbufu waumini wanaohitaji kwenda Hijjah.
Akizungumzaia suala la maadili wakati huu wa sikukuu
ya Eid el Fitri, Al hajj Dk. Mwinyi ameihimiza jamii kuendeleza maadili ili
kujiepusha na vitendo viovu vikiwemo uvunjifu wa amani, udhalilishaji, rushwa,
ubadhirifu na dhulma.
Pia aliwaasa wananchi kuendelea kuheshimiana, kutii
sheria za nchi, kuwa waadilifu, washirikiane pamoja na kuiendeleza amani
iliyopo kwa umoja na mshikamano baina yao.
Al hajj Rais Dk. Mwinyi, alisema kwa nyakati
tofauti jamii zimekua zikikumbushwa kuhusu umuhimu wa kuendeleza maadili ili
kupata mustakbali wa jamii njema.
Aliongeza suala la
kuporomaoka kwa maadili bado linaitesa jamii na kuchangia kuzorotesha juhudi za
maendeleo kwenye ustawi wa jamii.
Vile vile, Al hajj
Mwinyi aliinasihi jamii kuendelea kupiga vita mambo yasiyoendana na maadili,
mila, silka na tamaduni za Wazanzibari ili kupata kizazi kilichoongoka.
“Tuendelee kushirikiana katika
kuyapiga vita mambo haya, hayaendani na maadili mema, silka na utamaduni
walioachiwa na wazee wetu,” alisisitiza Al hajj Mwinyi.
Akizungumzia suala la malezi, Al
hajj Dk. Mwinyi aliwaasa
wazazi, walezi na wazee kuhakikisha wanasimamia malezi ya watoto wao ili wawe
waumini bora na raia wema wa kwa nchi yao pamoja na kuwasimamia kupata haki yao
ya elimu ikiwemo elimu ya dini pamoja na kulinda usalama wao dhidi ya mambo
yanayoweza kuwadhuru.
Sambamba
na hayo aliwahimiza wazazi/walezi kuzingatia usalama wa watoto wao hasa wakati
huu wa sikukuu kwani ni wajibu wao kuwasimamia na kuhakikisha wapo salama dhidi
ya mambo yote yanayoweza kuharibu furaha na amani yao pamoja na wazazi wao.
“Wajibu
huu tuubebe sote kwa kuhakikisha watoto wetu wanatoka majumbani na wanarejea
wakiwa salama.
Mapema asubuhi, Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi, alijumuika na waumini wa dini ya Kislam kwenye sala ya Iddi Fitri iliyosaliwa msikiti wa Masjid Zinjibar Kiembesamaki.
Pia alipata fursa ya kuzungumza na mashehe kutoka maeneo mbalimbali ya Zanzibar waliofika Ikulu, Zanzibar kwaajili ya kumtakia salam ya heri ya Eid el Fitri.
Katika halfa hiyo, Al hajj Dk.
Mwinyi pia aliwaasa Mashehe hao kuendelea kuwaelekeza wananchi kuhusu masuala
ya maadili, kuendeleza mashndano ya Qur’an alisema mambo yote yaliyokua
yakifanywa kwnye mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan yaendelezwe kwenye miezi
mingine inayoendelea pamojana kuendelea kuhimiza amani ya nchi kwa waumini
wote.
Kwenye hafla ya Baraza la Eid,
viongozi mbalimbali wa Serikali na siasa walihudhuria wakiwemo Marais wastaafu
wa Zanzibar awamu ya sita Dk. Amani Abeid Karume, Dk. Ali Mohamed Shein, Rais
wa awamu na saba, Makamu wa Kwanza wa Rais, Othman Masoud Othman, Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah, Spika wa Baraza la
Wawakilishi Zubeir Ali Maulid, Mufti Mkuu wa ZanIbar, Shekh Saleh Omar Kabi,
Jaji Mkuu wa Zanzibar, Khamis Ramadhan Shaaban, Mwenza wa Rais wa Jamuhuri ya
Muungano wa Tanzania Hafidh Ameir na Mawaziri na Manaibu mawaziri na
viongozi wengine wastaafu wa Serikali.
IDARA YA MAWASILINO, IKULU ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment