Habari za Punde

Mpango Mkakati wa Elimu ya Mazingira Waiva

 

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano Na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amesema Serikali ipo kwenye hatua za mwisho za kukamilisha Mpango Mkakati wa kutoa Elimu kwa Umma wa miaka mitano (2022/23-2026/27).

Amesema lengo la Mpango mkakati huo ni kuhamasisha umma wa Tanzania kuhusu maendeleo endelevu pamoja na uhifadhi wa mazingira. 

Mhe. Khamis ametoa kauli hiyo leo Mei 19, 2023 wakati akijibu swali la Mbunge wa Segerea Mhe. Bonnah Kamoli aliyeuliza mpango wa Serikali wa kuwapa elimu ya utunzaji mazingira wananchi wanaofanya shughuli za kilimo katika vyanzo na njia za mito ili wafanye kilimo bila kuleta athari za mazingira.

Naibu Waziri amefafanua kuwa Mkakati huo wa elimu umehusisha namna ya utoaji elimu kuhusu matumizi ya ardhi ndani ya Mita 60 katika maeneo ya vyanzo vya maji.

“Licha ya Serikali kuruhusu wananchi kufanya shughuli za kilimo kwa umbali wa mita 60 katika maeneo ya vyanzo vya maji, bado kuna changamoto nyingi za uharibifu mkubwa wa mazingira,” amesema.

Hivyo, kutokana na changamoto hiyo Mhe. Khamis ametoa wito kwa viongozi wa kisiasa naomba nichukue fursa hii kuwaomba viongozi wa kisiasa kutumia uwezo wa ushawishi walionao kuhamasisha jamii zinazofanya shughuli za kiuchumi katika maeneo ya vyanzo vya maji kuhifadhi mazingira.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.