NA MWASHAMBA JUMA
MWENYEKITI wa Taasisi ya “Zanzibar Maisha Bora
Foundation’ (ZMBF), Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Mama Mariam Mwinyi ametoa wito kwa jamii kuzingatia suala la
Usalama wa Chakula ili kujikinga na maradhi yatokanayo na chakula kisicho
salama.
Mama Mariam Mwinyi aliyasema hayo, kwenye
maadhimisho ya siku ya kimtaifa ya Usalama wa chakuka yaliyofanyika, viwanja
vya Mwembekisonge, Wilaya ya Mjini.
Alisema kumekua na ongezeko la maradhi
yanayosabishwa na usalama mdogo wa chakula, jambo alilolieleza kuathiri afya kwenye
jamii.
Aliiasa jamii, kula vyakula vilivyo
salama kwa kufuata mtindo mzuri wa kula pamoja na kufanya mazoezi ili
kuipunguzia Serikali mzigo mkubwa wa matibabu.
Mwenyekiti huyo wa (ZMBF) alieleza moja ya lengo
la kuanzishwa kwa taasisi ya “Zanzibar Maisha Bora Foundation” ni kuona namna
bora ya kuunga mkono jitihada za Kitaifa na Kimataifa kwenye suala zima la kuimarisha
lishe, afya na ustawi wa Wazanzibari ili kukuza maendeleo ya kiuchumi hususan
kwa wanawake, watoto na vijana.
Alisema siku
ya Usalama wa Chakula duniani ni jambo jema linaloleta uwelewa mpana juu ya
mambo yanayohusu usafi na usalama wa chakula katika kupunguza maradhi na
kuimarisha uchumi wa Zanzibar.
Hivyo, aliwasihi
watunga sera,
Mamlaka ya Usalama wa Chakula, wanasayansi, wakulima, wauzaji wa chakula,
wapishi, walimu, wanafunzi na watumiaji mbalimbali, kuongeza bidii za pamoja
ili kuhakikisha mwamko wa Usalama wa Chakula unaongezeka, Zanzibar.
Pia, Mama Mariam aliwataka watunga Sera
na waratibu kuhakikisha wanazingatia sera za udhibiti wa mifumo kwa usalama wa
chakula na kuimarisha ushirikiano wao kwa wadau wote na kuhakikisha wanaifahamu
miongozo na kuitumia mifumo iliopo katika juhudi za kumlinda mlaji.
Aidha, aliwaasa wafanyabiashara za
chakula kwamba wana jukumu la kufuata maelekezo ya viwango vilivyotolewa na
mamlaka na kuwaeleza kuwa jukumu la kumlinda mlaji limo mikononi mwao.
Aliisisitiza
jamii suala la Usalama wa
Chakula ni pamoja na kuzingatia kula mlo uliotimia ili kupata lishe bora zaidi
kwa watoto, wazee na wajawazito kwa kuimarisha mfumo wa kinga ulio imara na
makuzi mazuri kwa watoto.
“Tujitahidi kula chakula kilicho safi
kwa kuzingatia virutubisho na wingi unaofaa au unaohitajika”. Alisisitiza Mama
Mariam
Wakati huo
huo, Mama Mariam Mwinyi, aliupongeza uongozi wa Wizara ya Afya na wa Wakala wa Chakula
na Dawa kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya kwa kudhibiti vyakula
vinavyoingia na vile vinavyozalishwa nchini kwa kuhakikisha kuwa salama kwa
matumizi ya binaadamu.
“Kwa hakika, ukaguzi mnaoufanya kwenye
maeneo yanayouzwa vyakula na kuwepo kwa Maabara za kisasa za ZFDA hufanya
tujiamini juu ya bidhaa za vyakula zilizopo kwenye soko la Zanzibar kuwa ni
salama kwa matumizi ya binaadamu”. Alisifu Mama Mariam.
Mapema akizungumza kwenye hafla hiyo,
Waziri wa Afya, Nassor Ahmed Mazurui alisema, Wizara kupitia taasisi zake
wanaweka taratibu bora za kudhibiti vyakula vibovu visiingie nchini.
“Tuhakikishe tunakula vyakula bora,
usafi wa mazingira na uzalishaji wake, kwa bidhaa zote za mashambani na kwenye
mifugo” Alisisitiza Waziri Mazurui.
Pia, aliitaka jamii, kufuata taratibu
za kuvuna mara baada ya umwagiliaji na kupigwa dawa kwa mazao na Wanyama.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji kutoka Wakala
wa Chakula, Dawa na Vipodozi (ZFDA) Dk. Burhan Othman Simai alisema, jukumu
kubwa la taasisi hiyo ni kulinda afya ya jamii katika kuhakikisha bidhaa za
chakula, dawa, vipondozi, vifaa tiba na vitendanishi vina ubora, usalama na
ufanisi unaotakiwa kwa mujibu wa viwango vya kitaifa na kimataifa.
ZFDA ilianzishwa mwaka 2006 na
kufanyakazi rasimi mwaka 2007 kwa mujibu wa Sheria ya Chakula Dawa na Vipodozi
Sheria no 2/2006 na marekebisho yake, sheria no 3/2007.
Maadhimisho ya siku ya kimtaifa ya Usalama wa chakuka yenye kauli mbiu, “Usalama wa chakula ni jukumu la kila mmoja wetu”awali yaliambatana na mtembezi ya kilomita tano yaliyoongozwa na Mwenyekiti wa “Zanzibar Maisha Bora Foundation”, Mama Mariam Mwinyi, kutoka soko la mbogamboga Mombasa hadi viwanja vya Mwembe kisonge.
No comments:
Post a Comment