Habari za Punde

TANZANIA NA ALGERIA KUSHIRIKIANA KATIKA SEKTA YA VIJANA NA MICHEZO

 

Na Shamimu Nyaki

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana pamoja na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Tabia Maulid Mwita leo Juni 3, 2023 Jijini Algiers nchini Algeria wamekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Vijana na Michezo wa nchi hiyo Mhe. Abderrahmane Hammad

Mazungumzo hayo  ambayo pia yamehudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini humo Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu yamefanyika katika ofisi za wizara hiyo, ambapo kwa pamoja wamekubaliana kuundwa kwa Timu Maalumu ya Wataalamu ( Task Force) itakayohusisha wataalamu kutoka Tanzania Bara na Zanzibar kwa lengo la kuainisha maeneo ya kimkakati ya ushirikiano baina ya nchini hizo mbili kwenye sekta za Vijana  na Michezo.

 Aidha, Mawaziri hao wamekubaliana  kubadilishana uzoefu wa kitaalamu katika Sekta hizo kwenye maeneo yatakayoainisha na timu ya wataalamu.

Mazungumzo hayo pia yamehudhuriwa na Katibu Mkuu wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Bi. Fatma Hamad Rajab na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Nicholas Mkapa.




No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.