Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla amewakumbusha waumini wa dini ya kiislam na wananchi wote kuwa miongoni mwa neema kubwa kwa mwanaadamu ni kuwa na wazazi wawili ambao tunapaswa kuwatendea wema wakiwa hai na kuwakumbuka kwa duwa watakapotangulia mbele ya haki
Akiwasalimu waumini wa Masjid Tawbah Kisauni katika Ibada ya Sala ya Ijumaa, Alhajj Hemed amesema kuwafanyia wema wazazi wawili ni miongoni mwa ibada kubwa ambayo hujenga mahusiano mazuri baina ya wazazi na watoto wake na kuongeza mapenzi katika Familia.
Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameeleza kuwa Uislamu umehimiza suala la maendeleo hivyo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imedhamiria kurahisisha huduma katika sekta ya Afya ikiwemo ujenzi wa Hospital pamoja na kukabidhi Kampuni Binafsi kwa ajili ya utoaji wa huduma za maabara.
Aidha, amewataka wananchi waendelee kumuunga Mkono Rais iwa Zanzibar Alhajj Dkt Hussein Ali Mwinyi pamoja na Serikali anayoiongoza kwani dhamira yake ni njema kwa wananchi wake ikiwa ni pamoja na kusimamia maslahi yao na kuwawekea mazingira bora kiuchumi na kijamii.
Alhajj Hemed amesema Serikali ipo mbioni kukamilisha utaratibu wa kuwapatia Stahiki zao waathirika wa Benki ya FBME na kuwataka wananchi wawe na subira wakati Serikali ikikamilisha taratibu hizo
Akitoa Khutba ya Sala ya Ijumaa Shekh Masoud Mtumwa Khamis amewataka wazazi na walezi kusimamia malezi ya watoto wao na kukemea tabia ya baadhi ya wazazi kuwatelekeza watoto hatua ambayo inapelekea watoto hao kukosa malezi ya karibu ya wazazi wao.
Aidha ameeleza kuwa ni wajibu wa waumini wa Dini ya Kiislamu na wananchi kwa ujumla kuunga Mkono juhudi za Serikali hasa katika kupinga matendo ya udhalilishaji, rushwa na matumizi ya madawa ya kulevya vitendo ambavyo vinachangia kupotea kwa nguvu kazi ya Taifa letu.
Imetolewa na kitengo cha habari (OMPR)
Leo trh. 30.06.2023
No comments:
Post a Comment