RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,
Dk. Hussein Ali Mwinyi, amezionya taasisi za Serikali zinazokwepa matumizi ya
mabadiliko ya mifumo ya kisasa kwenye utendaji wao.
Alisema, kuna baadhi ya taasisi zinakiuka matumizi
na miongozo ya mifumo iliyowekwa kisheria kwa utekelezaji na utendaji wa kazi zao,
jambo alilolikataza mara moja kwani linakwamisha mipango na malengo ya Serikali.
Dk. Mwinyi aliyasema hayo ukumbi wa Golden
Tulip, Uwanja wa ndege Mkoa wa Mjini Magharibi kwenye uzinduzi wa Mkakati wa
Kidijitali wa Serikali na Mfumo wa kitaifa wa Bajeti na Matumizi Serikalini
(BAMAS).
Aliwaagiza viongozi
wa taasisi hizo wakiwemo Makatibu
wakuu na wakuu wa taasisi wanazozisimamia kuhakikisha wanapokea na kutumia mifumo
ipasavyo kwa lengo la kujenga na kuimarisha miundombinu ya TEHAMA, sheria,
miongozo, pamoja na taasisi zilizopewa majukumu ya kusimamia masuala hayo.
“Nawaagiza viongozi wote wa Wizara, Idara,
Taasisi za Serikali zote ikiwemo Mashirika na Taasisi za Kodi, Serikali Kuu na
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kulisimamia agizo hili mara moja.”
Aliagiza Rais Dk. Mwinyi.
Dk, Mwinyi alisema, Serikali itapunguza
hujuma zinazofanywa na wachache kwa kutumia hati na nyaraka za kughushi na
kuongeza mifumo imara, itatoa taarifa zilizotibitishwa kidijitali.
Aliwaagiza Wakala wa Serikali Mtandao kupitia
Ofisi ya Rais - Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora kushirikiana na Ofisi
ya Rais - Fedha na Mipango, kutoa elimu kwa taasisi zote za Serikali na wananchi
juu ya mkakati wa pamoja na matumizi ya Mifumo mipya ya serikali inayoendelea
kuzinduliwa.
Alieleza, mfumo huo pia
utaimarisha sekta muhimu za kiuchumi, uwekezaji na ukusanyaji wa mapato nchini
kwa kuzingatia mbinu na mikakati ya kuimarisha na kuendeleza sekta za utalii,
uchumi wa buluu, kuharakisha utoaji wa huduma bora za jamii, ikiwemo bima ya
afya, kuimarisha biashara hasa kwa raia wageni hawatolazimika kufika Ofisi za
Serikali kufanya miamala au usajili wa biashara na kampuni zao badala yake popote
walipo watafanya hivyo kwa muda mfupi kupitia njia za kidijitali.
Pia Rais Dk. Mwinyi
aliongeza mfumo itarahisisha shughuli za usajili wa wanafunzi kwenye Skuli na
vyuo vikuu, usajili wa ndoa, vizazi na vifo.
Mfumo wa BAMAS pia umeondoa changamoto za mifumo
inayoendelea kutumika sasa ya ukusanyaji mapato (Isidore) na Mfumo wa Matumizi
(Epicor) na kueleza kwamba BAMAS umeleta uwazi kwenye Bajeti na Matumizi
Serikalini kwa kuwezesha Mifumo yote ya Malipo na Matumizi ya Fedha za Serikali
kusomana kwa haraka na kwa ufanisi.
Alieleza matarajio yake kwa Mfumo wa BAMAS kwamba utaongeza nguvu ya udhibiti wa mali za Serikali, uwajibikaji kwa Watumishi na watendaji wa Umma na kuhakikisha fedha za Umma zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa, ili kuwaletea wananchi maendeleo.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Nchi
Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, Dk. Saada Mkuya Salum, alisema Mfumo wa BAMAS
utaongeza ufanisi na utoaji wa huduma bora za Serikali pia utaunganisha pamoja
sehemu ya mapato na matumizi ya Serikali.
Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba
Sheria, Utumishi na Utawala Bora, aliiomba Serikali kuiongezea uwezo taasisi ya
wa badala ya kuwa wakala kuwa Mamlaka ili kuiongezea ufanisi na usimamiaji
mzuri wa matumizi mtandao kwa taasisi zote za Serikali.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala
Serikali Mtandao Zanzibar, Saidi Seif Said alieleza kwa kipindi cha miaka
miwili na nusu sasa wametengeneza na kusimamia mifumo 28 ukiwemo mfumo wa BAMAS
na kueleza kwelekeo wa taasisi hiyo ni kuongeza kasi ya kutengeneza mifumo
yenye nguvu zaidi ili kuongeza ufanisi wa kiutendaji kwa taasisi za Serikali.
Uzinduzi wa Mkakati wa Kidijitali wa Serikali
na Mfumo wa Bajeti na Matumizi Serikalini (BAMAS) ulikwenda sambamba na
kaulimbiu “Hatma yetu ipo viganjani mwetu”
IDARA YA MAWASILIANO, IKULU-ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment