Habari za Punde

Vikundi 130 mradi wa Viungo kupatiwa Simu kurahisisha kazi zao


Afisa mwezeshaji vikundi vya hisa mradi wa Viungo Lalo Kukas akiwaelekeza wakuu wa vikundi vya hisa  jinsi ya kutumia mfumo maalum (CHOMOKA)  katika simu za kisasa (smartphone) wakati wa mafunzo  ya kuwajengea uwezo  wanavikundi hao  juu ya matumizi ya mfumo huo utakaowarahisishia kutunza kumbukumbu hafla iliyofanyika Ofisi za Viungo Mwanakwerekwe Zanzibar .PICHA NA FAUZIA MUSSA -MAELEZO ZANZIBAR     

Na Rahma Khamis Maelezo                  
Jumla ya Vikundi  130  vya hisa katika  mradi wa Viungo  wanatarajiwa kupatiwa Simu aina ya Samsung Galaxy S6  ili  kurahisisha kazi zao ikiwemo utunzaji wa  kumbukumbu Unguja na Pemba.

Akitoa mafunzo ya kutumia mfumo maalum ujulikanao kama CHOMOKA ( PDF VSLA DIGITAL MOBILE PLAT FORM) kupitia simu za kisasa huko Ofisi za Viungo Mwanakwerekwe Afisa Mwezeshaji  wa  Vikundi hivyo  Lalo Kukas  ambae pia Mwalimu wa vikuindu vya hisa vya jamii amesema kuwa mfunzo hayo yanalenga kuwatoa wakulima katika analojia na kuwapeleka katika digitali.

Amefahamisha kuwa awali wanachama hao walikua wakitunza taarifa za hisa  katika vitabu jambo ambalo lilirejesha nyuma harakati zao kwani taarifa nyingi zilipotea hivyo kupitia mfumo huo wataweza kutunza kumbukumbu kwa uhakika hususani za hisa na mikopo.

Aidha amefahamisha kuwa mfumo huo utawafanya wanavikundi hao kutumia muda mfupi katika vikao na kuweza kutumia muda mwingi katika uzalishaji.

Vile vile Kukas alisema  kupitia mfumo huo kutaondoa migogoro ya taarifa tofauti za fedha kunakopelekea  vikundi vingi kuvunjika.

"Tumewaletea Simu hizi  kwa ajili ya kupunguza muda na kuwarahisishia kazi zenu ikiwemo usajili wa wanachama, kufanya mahesabu pamoja na kutunza kumbukumbu za kuweka na kukopa ",alifahamisha Afisa.

Afisa Kukas ameeleza kuwa katika  kuhakikisha  vikundi hivyo vinaondokana na matumizi ya kizamani mradi umeamua kuwawaezesha kwa kuwapatia simu aina ya  Samsung Galaxy  S6  bila ya malipo ambazo watatumia kwa ajili ya shuhuli zao kwa kila kikundi ambacho kipo chini ya mradi wa viungo.

Akitolea ufafanuzi juu ya mradi huo amesema mradi ni  wa miaka minne na sasa wapo katika mwaka wa tatu ambapo hadi kufifikia  mwisho wa mradi wanatarajia kuviifikia vikundi 200  Unguja na Pemba .

Nao washiriki wa Mafunzo hayo wamesema  kupitia mradi wa viungo wanategemea mabadiliko zaidi kwani bado wanaendelea kujifunza na kuwashauri Vikundi vyengine kujiunga katika mradi huo ili kuweza kutatua changamoto zinazojitokeza katika vikunndi ikiwemo kupotea kwa vitabu.

Mafunzo hayo  ya siku tano na yalishirikisha vikundi vya hisa kutoka Wilaya zote za Unguja.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.