Habari za Punde

Wahudumu wa Afya wapatiwa mafunzo ya kutibu maji

Afisa Afya kutoka kitengo cha Afya na Mazingira Zanzibar Fuad Othman akizungumza na wahudumu wa Afya wa kujitolea  (CHV) wa shehia ya Mjini na Magharibi "A" wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wahudumu hao  juu ya kutibu maji huko Skuli ya Magufuli Mwanakwerekwe Zanzibar julai 15,2023.PICHA NA FAUZIA MUSSA -MAELEZO ZANIZBAR

Na Rahma Khamisi Maelezo


Jamii imetakiwa kuhakikisha kuwa maji wanayotumia kwa ajili ya  kunywa  yako salama ili kujikinga na maradhi ya mripuko ikiwemo kipindipindu.


Akitoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wahudumu wa Afya wa kujitolea (CHV) juu ya  kutibu maji  katika Skuli ya John Magufuli Mwanakwerekwe Afisa Afya Kitengo cha Mazingira kupitia Wizara ya Afya  Fuwad Othman amesema  kutibu maji ni jambo muhimu kutokana na kulinda afya ya mtumiaji kwani kuna baadhi ya watu wanatumia maji ya kunywa yasiyo salama.


Akielezea  baadhi ya  njia za kutibu maji amesema ni pamoja nakuyachemsha kwa dakika 2 au kutumia kidonge cha  Watergard kuulia vijidudu vilivyomo ndani ya maji hayo.


"Tujitahidini jamani tuhakikishe maji tunayokunywa yawe salama kwani maji yetu tunayotumia  wakati mwengine huwa yanachafuka kwa kuingiwa na vitu tofauti ambavyo haviko salama alisisitiza Afisa huyo" .


Aidha amefahamisha kuwa awali wahudumu wa Afya walitumia kidonge kimoja cha watergurd kuulia vijidudu  katika ndoo ya maji  ya lita 5,hivyo baada ya uchunguzi afisa huyo aliwataka kutumia kidonge hicho kwa ujazo wa lita 20.
Aidha amefahamisha kuwa ili maji yaendelee kuwa  salama lazima yahakikishe yamehifadhiwa kwa kufunikwa .


"Njia zote hizo ni muhimu lakini njia ambayo ni bora zaidi ni ya kutibu kwa tia dawa  (wate guard) Skwa sababu njia hiyo ni nzuri na haina mashaka ." amefafanua Afisa huyo.


Katika hatua nyingine Afisa Mazingira amesema kuwa Maafisa wa Afya na mazingira wamekuwa wakipitia visima vya Zawa mara kwa mara kuangalia usalama wa maji lakini haitoshi hivyo ni vyema jamii iendelee kuyatibu maji hayo  kuwa salama zaidi.


"ikiwa maji yametibiwa kwenye Tangi la ZAWA hata yakae siku tatu maji yanakuwa yapo salama kwani kuna maafisa wetu  wanatembelea kila baada ya muda kuangalia kiwango cha dawa  kilichokuwemo kinakubalika au laa lakini   maji yakitoka  mferjini huwa ni machafu kwani anapitia sehemu mbalimbali hivyo hayafai kwa kunywahadi yatibiwe tena ,alifahamisha"


Hata hivyo alitumia fursa hiyo kuwaomba wafanya biashara wa mikahawa kutibu maji  ili kuuwa vijidudu kabla ya kutumiwa na kuleta madhara kwa mtumiaji.


Nao wahudumu wa Afya wa kujitolea wamesema kuwa maji ya Zawa huwezi kuyathibitisha kama yapo salama mpaka yapimwe hivyo ipo haja ya jamii kupatiwa elimu zaidi ili kuweza kupata usaalama wa Afya.


Aidha wameomba kupatiwa vitambulisho  maalum ili kuweza kutambulika  wanapofika katika jamii  kwani kuna baadhi yao huwapuuza wakati wanapofika kwa ajili ya kuwapatia elimu .


Mafunzo hayo ni ya siku mbili na yamewashirikisha wahudumu wa Afya zaidi ya 150 kutoka Wilaya zote za Mkoa wa Mjini Magharibi.
 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.