Bank of Africa -Tanzania Limited imezindua huduma za wakala za kibenki zinazoitwa ‘Bank of Africa WAKALA’ kwa lengo la kuboresha ukaribu na wateja wake na kuongeza mtandao wa wateja kote nchini.
Mfumo huu mpya unaiwezesha BANK OF AFRICA, kuingia mkataba na mawakala wa kampuni ya Selcom nchini pote kuweza kutoa huduma za kifedha Kwa niaba yake.
Akiongea wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji na Afisa Mtendaji Mkuu wa BANK OF AFRICA-TANZANIA LIMITED, Bw. Adam Mihayo alisema, “Haya ni mafanikio makubwa kwa benki hii, tunapoendelea na safari ya kuelekea kuweka bidhaa na huduma zetu katika mfumo wa kidijitali, na hivyo kuwarahisishia wateja wetu kupata huduma mahali popote na wakati wowote mbali na kutumia mtandao wa matawi yetu wa siku zote”.
“Tunapozindua huduma mpya leo huduma zetu za kifedha zitapatikana kwa mawakala 100 nchini pote kwa awamu hii ya kwanza , na mawakala wengine 200 wataongezeka katika awamu ya pili. Haya ni mafanikio makubwa katika kupeleka huduma za kibenki kwa wananchi wa Tanzania, benki bado ina dhamira ya dhati ya kuendeleza ajenda ya uchumi wa nchi kupitia uwekezaji mbalimbali unaofanywa na tunaendelea kuwekeza”.
Mkuu wa Huduma za Dijitali wa Benki hiyo, Bw. Jesse Jackson, alieleza kuwa huduma hii imeanzishwa kwa ajili ya kukidhi na mahitaji ya soko na kuhakikisha huduma za kifedha zinapatikana katika maeneo mengi zaidi. "Lengo letu linatokana na mkakati wetu wa kuongeza ujumuishaji wa kifedha na hitaji la kuendesha mifumo ya kidijitali inayowawezesha wateja wetu kupata huduma za kifedha moja kwa moja katika maeneo yao, Bank of Africa WAKALA inaleta urahisi kwa wateja wetu kwa kutuma na kuweka fedha kwa kuanzia".
"Uzoefu wa kipekee kwa wateja ni muhimu kwetu kama BANK OF AFRICA, tunataka wateja wetu wajisikie wamekaribishwa sio tu kwenye kumbi za benki bali kwenye maeneo mengine wanayoishi. Tunataka kuanzisha uhusiano na kila mtu anayestahili kupata huduma za kibenki bila kujali kiwango cha kipato chake au hali yake na huduma za kidigitali ni moja ya nguzo muhimu zilizopo katika malengo ya kimkakati ya benki katika mpango mkakati wetu, ubunifu zaidi bado unakuja tunapoelekea kufanikisha lengo hili,” alisema Jesse.
Kwa kuzindua mfumo huu wa Mawakala, benki pia inaongeza idadi ya wadau katika mnyororo wa thamani wa mfumo wa kifedha hivyo basi kutengeneza nafasi za ajira na kiuchumi kwani inatoa viwango vya kamisheni vizuri kwa WAKALA wake.
Bw. Jesse Jackson alisisitiza kuwa mwelekeo wa kimkakati wa Benki, BANK OF AFRICA-TANZANIA imedhamiria kutoa huduma mbalimbali za kidigitali kwa wateja wake sio tu zinazoendana na matakwa yao,mtindo wao wa maisha na mahitaji yao ya huduma za kifedha , na zinaleta uzoefu wa kipekee wa wateja.
Nia ni kukidhi mahitaji yote ya makundi yote ya wateja wetu, kusaidia ujumuishaji wa kifedha na kutoa jukwaa kwa watu wote kupata huduma za benki.
No comments:
Post a Comment