Habari za Punde

Dk Mwinyi akutana na Kaimu Mkurugenzi Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Ofisi ya Zanzibar Ikulu

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akimsikiliza Kaimu Mkurugenzi Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Ofisi ya Zanzibar, Balozi Silima Kombo Haji alipofika Ikulu Jijini Zanzibar leo Kujitambulisha.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amehimiza ushirikiano wa karibu baina ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Serikali ya Mapindizi ya Zanziar.

Dk. Mwinyi ameyasema hayo Ikulu, Zanzibar alipozungumza na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afika Mashariki, Zanzibar Balozi Silima Kombo Haji aliefika kujitambulisha.

Rais Dk. Mwinyi alisema taasisi mbili hizo zinategemeana kwenye ushirikiano wa majukumu yao hasa kwenye masuala yanayohusu mambo ya kimataifa.

“Mara zote tumekua tukiihitaji ushirikiano na ofisi hii (Idara ya Mambo ya Nje, Zanzibar) hasa kwa mambo ya kimataifa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar milango yetu ipo wazi kutoa ushirikiano na ofisi yenu, kama kukiwa na changamoto yoyote usisite kutupa taarifa na tutaitatua kwa hatua kwa kukupa ushirikiano unaostahili ili utimize majukumu yako” Dk. Mwinyi alimuahidi Balozi huyo.

Aidha, alimtaka Balozi Silima ambae pia ni Baloizi wa Tanzania nchini Sudan kwa kuwa kiungo mzuri kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye eneo la ukanda wa Afrika Mashariki na Kimataifa.

Pia, Rais Dk. Mwinyi alimpa pole Balozi huyo kwa matatizo waliyoyapata kituoni kwao Sudan wanakoiwakilisha Tanzania kimataifa kutokana na changamoto za vita zinazoendelea nchini humo.

Dk. Mwinyi, alitumia fursa hiyo kumkaribisha nyumbani Tanzania, kuendeleza majukumu yake ya ujenzi wa Taifa na kulitakia heri taifa la Sudan kwa kuliombea kurejea kwenye amani yao ya zamani.

Naye, Balozi Silima alimuahidi Rais Dk. Mwinyi ushurikiano wenye tija katika utekelezaji wa majukumu yao ya kusimamia huduma za Diplomasia na Itifaki katika kukuza ushirikano wa Kimataifa na kikanda kwa nyanja zote za uchumi na siasa.

Balozi Silima alimuhakikishia Rais Dk. Mwinyi kwamba atayatekeleza vema majukumu yake kwa uaminifu na juhudi kubwa kwa kutumia taaluma aliyonayo, uzoefu na juhudi zake kuyafanikisha.

Sambamba na kumuahidi kutekeleza maelekezo atakayotoa kwa Idara ya Mambo ya Nje, Zanzibar kuyafanikisha kwa ufanisi na weledi wa hali ya juu hasa kwenye suala zima la ushirikiano baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mapinduzi ya Zanzibar na kumueleza kuwa tayari wakati wote kwa utekelezaji.

Aidha, Balozi Silima alimshukuru Rais Dk. Mwinyi kwa nasaha na maelekezo yake na kumuahidi kuwa yatakua mwanga mzuri na dira kwa Zanzibar na nyanja za kimataifa.

Kaimu Mkururugenzi Idara ya Mambo ya Nje, Zanzibar ana jukumu la kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afika Mashariki kwa Zanzibar kutoa huduma za Diplomasia na itifaki kwa masuala ya kitaifa, kanda na kimataifa.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (katikati) akizungumza na Kaimu Mkurugenzi Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Ofisi ya Zanzibar, Balozi Silima Kombo Haji (kushoto) alipofika Ikulu Jijini Zanzibar leo Kujitambulisha (kulia) Wasaidizi wa Rais 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi akiwa katika picha na  Kaimu Mkurugenzi Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Ofisi ya Zanzibar, Balozi Silima Kombo Haji (kushoto) alipofika Ikulu Jijini Zanzibar leo Kujitambulisha.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akiagana na  Kaimu Mkurugenzi Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Ofisi ya Zanzibar, Balozi Silima Kombo Haji baada ya Mazungumzo alipofika Ikulu Jijini Zanzibar leo Kujitambulisha 
.[Picha na Ikulu]28/08/2023. 


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.