Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar Mheshimiwa Suleiman Masoud Makame amekutana na Kampuni ya Kimataifa ya Schlumberger (SLB) kutoka Uingereza kwa ajili ya kuzungumzia mwelekeo wa muendelezo wa kazi ya utangazaji wa vitalu vya mafuta na gesi asilia kwa wawekezaji wa sekta hiyo.
Katibu Mkuu Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Dkt. Aboud Suleiman Jumbe ameishukuru Kampuni hiyo ya SLB kwa kuendelea kutoa mashirikiano chanya kwa Zanzibar katika kuitangaza Zanzibar na vitalu vyake kwa uwekezaji pamoja na uwezeshaji katika kukuza na kuendeleza sekta ya mafuta na gesi asilia Zanzibar.
Alisema Dkt. Aboud tayari Kampuni ya SLB na Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi kupitia Mamlaka ya Udhibiti na Utafutaji wa Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar (ZPRA) pamoja na Kampuni ya Maendeleo ya Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar (ZPDC) kwa pamoja zipo katika hatua za mbali za kuitangaza Zanzibar kwa mkakati wa kibiashara na uwekezaji ( Non Technical Strategy) ya kuhakikisha wawekezaji wanakuja na kutumia fursa za vivutio vilivyotangazwa na Serikali ikiwemo marekebisho mbali mbali ya kisheria na kiuwekezaji.
Wakati huo huo mtaalamu wa miamba wa Kampuni ya SLB Bwana Mohammed El Touqy amesema wataendelea kutoa mashirikiano huku wakiendelea kuitangaza Zanzibar kimataifa zaidi ili kufanikisha lengo la kupata wawekezaji wa kimataifa.
Mchakato wa kuvitangaza na kuvigawa vitalu kwa wawekezaji kwa mashirikiano na Kampuni ya SLB unaendelea.
No comments:
Post a Comment