RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali
Mwinyi, amesema ujio wa nyota maarufu wa filamu nchini China, Jin Dong,
utaendelea kuifungulia Zanzibar soko la Utalii kutoka China.
Dk.
Mwinyi ameyasema hayo Ikulu, Zanzibar alipotembelewa na msanii huyo ambaye yupo
Zanzibar kwa kazi ya kutengeneza filamu.
Alisema,
ujio wake ni fursa adhimu kwa Zanzibar kutangazwa kimataifa hasa kupitia Sekta
ya Utalii ambayo ni Sekta mama ya uchumi wa Taifa.
Rais
Dk. Mwinyi alimueleza mgeni wake huyo, kwamba Zanzibar ina vivutio vingi vya
Utalii, ukiwemo Utalii wa fukwe safi nyeupe zinazovutia wengi duniani, Utalii
wa utamaduni, Utalii wa Mji mkongwe, Utalii wa michezo, Utalii wa visiwa pamoja
na wa Mikutano.
Aidha,
alimkaribisha mgeni huyo kuitumia fursa ya kuwepo kwake Zanzibar kutembelea
maeneo muhimu ya Utalii likiwemo shamba la viungo vya Zanzibar, Kisiwa cha
Mnemba, Kaskazini Unguja pamoja na Mji Mkongwe wa Zanzibar.
Naye,
nyota huyo wa Filamu nchini China, Jin Dong, alimueleza Rais Dk. Mwinyi furaha
yake ya kufika Afrika kwa mara ya kwanza tena ndani ya visiwa vya Zanzibar kwa
nchi za Afrika Mashariki.
Alisema,
mbali na Safari ya Sanaa hapa Zanzibar lakini pia ujio wake unaimarisha
uhusiano wa undugu na urafiki uliopo baina ya China na Tanzania ikiwemo
Zanzibar.
Aliahidi
kuwa balozi mzuri wa kuitangaza Zanzibar kwa Utalii na alieleza imani yake ya
kuwavutia Wachina wengi kuja kutalii visiwa vya Zanzibar.
Miongoni
mwa maeneo ya Utalii aliyotembezwa msanii huyo ni kisiwa cha Mnemba, Mji
Mkongwe maeneo ya Forodhani na Ngome Kongwe.
Jin
Dong ni nyota mkubwa China mwenye wafuasi wa mitandao ya kijamii zaidi ya
milioni 15. Mbali na kazi za Sanaa pia ni Mwanasiasa nai Naibu Mkurugenzi wa
kikundi cha Sanaa cha serikali cha utamaduni.
IDARA YA MAWASILIANO IKULU,
ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment