SERIKALI
ya Mapinduzi ya Zanzibar imeeleza dhamira yake ya kuboresha na kuendeleza
huduma za jamii kwa wananchi wake ikiwemo kuimarisha huduma za Afya, Elimu,
Maji Safi na Salama na kudumisha usafi wa mazingira.
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi
aliyasema hayo Ikulu, Zanzibar alipozungumza na Mwakilishi Mkaazi Mpya wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF)Bi.Elke Wisch aliyefika kujitambulisha.
Dk.
Mwinyi, alisema jitihada za Serikali kuendelea kuboresha huduma za jamii
ikiwemo miundombinu na rasilimali watu kwa kuwaendeleza wataalamu waliopo kwa
ustawi wa huduma hizo.
Rais
Dk. Mwinyi alisema Serikali pia inajivunia ushirikiano wake wa bega kwa bega na
Wadau wa Maendelo wakiwemo UNICEF pamoja na kusifu kazi kubwa zinazofanywa na
Shirika hilo katika miradi mbambali ya maendeleo iliyotekelezwa kuiunga mkono
SMZ.
“UNICEF
imefanya makubwa Tanzania hususani ushirikiano wa karibu na Wizara za SMZ inaungamkono
jitihada za Serikali yetu kwenye masuala mbalimbali ya maendeleo” alisifu Rais
Dk. Mwinyi.
Dk.
Mwinyi alimweleza Mwakilishi huyo kwamba, daima Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar itaendelea kuishukuru UNICEF kwa kuiunga mkono Zanzibar kwenye masuala
ya Afya na Elimu na yote yanayohusu ustawi wa watoto nchini.
Naye,
Mwakilishi huyo wa UNICEF, Tanzania Elke Wisch alishukuru ushirikiano uliopo
baina ya UNICEF na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hasa kwenye ustawi wa
masuala ya watoto na kuahidi kuendeleza ushirikiano huo.
UNICEF
ni Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) lililoanzishwa mwaka 1946 jijini New York,
Marekani, linashughulika na masuala ya Elimu na Watoto duniani, linafanyakazi
kwenye maeneo zaidi ya 190 duniani kote, katika kuwafikia watoto na vijana
walio kwenye matatizo kutokana na majanga mbalimbali kwa kuboresha chanjo kwa
watoto na kutoa lishe bora katika kuimarisha huduma za dharura mbali na mambo
mengine yanayowahusu watoto.
Mbali
na mambo mengi UNICEF iliyofanya kwa Zanzibar kupitia miradi mbalimbali ya Afya
na Elimu, Shirika hilo lilifanikiwa kwa asilimia 75 kuwarejesha skuli watoto
wengi walioacha masomo kwa mazingira tofauti waliyokumbana nayo kwenye makuzi
yao.
IDARA YA MAWASILIANO IKULU, ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment