RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Al
hajj Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameihimiza jamii kuendeleza malezi bora kwa watoto
na vijana ili kulinusuru Taifa na mporomoko wa maadili.
Al Hajj Dk. Mwinyi alitoa
nasaha hizo kwenye Msikiti wa Polisi Bomani, Mkoa wa Mjini Magharibi,
alikojumuika pamoja na waumini wa dini ya Kiislamu kwenye ibada ya sala ya
Ijumaa.
Alisema, siku hizi maadili yamepotea, jamii zimekithiri
vitendo visivyo na maadili mema kwa vijana ikiwemo wizi, watumiaji wa dawa za
kulevya, tofauti na zamani, hivyo aliwahimiza wazazi/walezi kuwalea vijana kwa
hofu ya kumuogopa Mwenyezi Mungu (S.W).
Alieleza, ndani ya jamii kuna mmong’onyoko wa
maadili, hivyo aliendelea kuiasa jamii kushirikiana kwenye malezi ya pamoja ili
kuwanusuru vijana na janga hilo.
Alieleza wazazi/ walezi wanawajibu wa kuhakikisha
makosa na mporomoko wa maadili hayafanyiki kwa vijana wao kwa kuendelea kuwa
wasimamizi wazuri kwao badala ya kusubiria vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua
hatua za kisheria, hivyo aliwahimiza kuendelea kuchukua tahadhari mapema.
Katika hatua nyengine, Al hajj Dk. Mwinyi aliisa
jamii kuendelea kuvumiliana na kuendeleza amani ya nchi licha ya tofauti za
kisiasa na imani zilizopo.
Alisema, ndani ya nchi
yenye watu wenye mitazamo na fikra tofauti haiwezekani wote wakakubaliana kwa
kila jambo, lakini kikubwa katika hayo ni kuvumiliana na kuelewana.
Aidha, Al hajj Dk. Mwinyi aliwaomba wanasiasa wa
vyama mbalimbali kupitia viongozi wa dini na waumini wao, kuendelea kubakia na amani
na uvumilivu kwani wakati mwengine kumekua kukijitokeza viashiria vya uvunjifu
wa amani kwa kutovumiliana kwenye jamii.
Katibu Mtendaji kutoka Ofisi ya Mufti Zanzibar, Sheikh Khalid Ali Mfaume aliwataka
waumini wa Dini ya Kiislam kuendelea kumuombea na kumtakia kheir Al hajj Dk.
Mwinyi kwani tokea ameingia madarakani amekua na ushirikiano mkubwa kwenye
jamii kwa kuendeleza utaratibu wake wa kushirikiana na jamii kwenye masuala ya
khairati ikiwemo kujumuika nao pamoja katika sala za Ijumaa kupitia misikiti ya
maeneo mbalimbali ya nchi.
Akihutubu kwenye sala
hiyo, Khatibu Sheikh Salum Othman Malolo aliiasa jamii kujiepusha na zinaa ya macho kwa kuangalia na ya
ulimi kwa kutamka machafu na kusifia maovu yanayofanyika kwenye jamii. Hivyo
aliitaka jamii kutozingatia na kujiepusha kutamani masuala machafu ya zinaa.
IDARA YA MAWASILIANO,
IKULU ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment