Habari za Punde

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali akagua miradi ya ujenzi atoa maagizo




Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mh. Lela Mohammed Mussa amesema kuwepo kwa Ofisi za kisasa za Elimu za Wilaya kutatoa fursa kwa Walimu Kutatua changamoto ya upatikanaji wa vitabu vya kufanyia maandalizi ya kufundishia.
Waziri Lela ameyasema hayo mara baada ya kukagua ujenzi wa vituo hivyo katika Wilaya ya Wete na Chake chake Pamoja na kutembelea miradi mbali mbali ya Ujenzi wa Skuli za Ghorofa Kisiwani Pemba.
Amesema ofosi hizo pia zitatoa huduma za maktaba hivyo Walimu watapata fursa ya kuzitumia maktaba hizo kupata vitabu vitakavyoweza kuwasaidia kufundisha kwa ufanisi.
Mh. Waziri amempongeza Mkandarasi wa Ujenzi wa Ofisi hizo Kwa kufanya kazi yenye kiwango kwa muda mfupi Zaidi ya mkataba unavyoelekeza.
Wakati huohuo Mh. Lela ametembelea miradi mbali ya ujenzi wa Skuli za Ghorofa ambapo ametoa maagizo kwa Mshauri mwelekezi kuchukua hatua za kisheria kwa Wakandarasi ambao watakwenda kinyume na mikataba yao.
Nae Mshauri Elekezi kutoka Wakala wa Majengo Zanzibar ZBA Said Malik Said amesema Wakandarasi ambao walionesha mapungufu sasa wameanza kufidia mapungufu hayo kwa kuongeza kasi utendaji kazi.
Amesema wakandarasi hao wameanza kufanya kazi kwa kasi na kwamba wameweka mikakati ya kufanya kazi usiku na mchana ili kufidia mapungufu yaliyojitokeza.
Kwa upande wake Muhandisi Msaidizi wa Kampuni ya SINIC CONSTRUCTION Ismail Mohammed Ali amesema Ujenzi wa Mradi wa Skuli ya Maziwang’ombe unaendelea vizuri licha ya changamoto mbali mbali zinazowakabili.


 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.