Habari za Punde

Mhe Othman afanya ziara maalum kukagua athari za kimazingira

 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman, akiongozana na Viongozi mbalimbali, alipowasili huko Shehia ya Mtoni Chemchem, Jimbo la Mwera, Wilaya ya Magharib A Unguja, kwaajili ya kukagua Daraja linalojengwa, jirani na Mtaro ambao ni tishio la mafuriko, katika maeneo hayo.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman (katikati), akiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Magharib A, Bi Suzane Peter Kunambi (wa mbele mwenye kilemba cheusi), alipowasili huko Shehia ya Mtoni Chemchem, Jimbo la Mwera, Wilaya ya Magharib A Unguja, kwaajili ya kukagua Daraja linalojengwa, jirani na Mtaro ambao ni tishio la mafuriko, katika maeneo hayo.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman, akipokea maelezo kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Mwera, Bw. Zahor Mohamed Haji, alipowasili huko Shehia ya Mtoni Chemchem, Jimbo la Mwera, Wilaya ya Magharib A Unguja, kwaajili ya kukagua Daraja linalojengwa, jirani na Mtaro ambao ni tishio la mafuriko, katika maeneo hayo.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman, akitoa maelekezo mbele ya Viongozi mbalimbali, alipowasili huko Shehia ya Mtoni Chemchem, Jimbo la Mwera, Wilaya ya Magharib A Unguja, kwaajili ya kukagua Daraja linalojengwa, jirani na Mtaro ambao ni tishio la mafuriko, katika maeneo hayo.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema ni vyema kuchukua juhudi za kila aina ili kuepusha majanga ya kimazingira katika jamii, yanayotokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.


Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo huko Shehia ya Mtoni Chemchem, Jimbo la Mwera, Wilaya ya Magharibi A Unguja, katika Ziara yake Maalum hapa Visiwani, akikagua Maeneo mbalimbali, yaliyopatwa na athari za kimazingira, kutokana na mabadiliko ya tabianchi.


Ameeleza hatari inayoikabili jamii na Taifa kwa ujumla, ikiwemo ya maafa kutokana na mitaro isiyokuwa salama, hasa kwa wakati huu unaokabiliwa na Indhari ya Wataalamu, juu ya ujio wa Mvua kubwa za Elnino, hapa Nchini.


Aidha Mheshimiwa Othman ameahidi kuwa Serikali ya Zanzibar kwa upande wake, itachukua hatua zote zinazostahiki, ili kuona kwamba Mazingira yanowazunguka wananchi, katika makaazi na maisha yao ya kila siku, yapo salama.


Hivyo, Mheshimiwa Othman ameuagiza Uongozi wa Jimbo hilo, kufanyakazi kwa mashirikiano na Mamlaka za Wilaya, Shehia na Jamii za Mtoni Chemchem, ili kuyalinda mazingira pamoja na Wananchi wanaoishi katika maeneo hayo, kutokana na maafa yanayoweza kuepukika, yanayotokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.


Naye, Mkuu wa Wilaya ya Magharibi A Unguja, Bi Suzane Peter Kunambi, akieleza matumaini wanayoyapata kutokana na Ziara za Viongozi wa Kitaifa, katika kutatua adha inayowakabili wananchi katika maeneo yao ya kuishi, ametoa wito kwa jamii kubadilika hasa katika kutekeleza usafi wa mazingira.


Amesema, kufuatia Ziara ya Mheshimiwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, katika Wilaya hiyo hivi karibuni, Uongozi wake umeamua kuanzisha Programu Maalum ya Usafi, ukiwemo wa Mitaro, na hivyo kuomba mashirikiano mema kutoka kwa wananchi, ili kuhakikisha Mpango huo unafanikiwa kwa kiasi kikubwa.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mazingira, Bw. Sheha Mjaja Juma, amewaasa wananchi kuepuka kuweka makaazi katika maeneo hatarishi, yanayoweza kukumbwa na athari za maafa ya kimazingira, zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.


Akieleza matumaini na juhudi za makusudi za kuwakinga wananchi kutokana na majanga hayo, Mbunge wa Jimbo la Mwera, Bw. Zahor Mohamed Haji, amebainisha dhamira ya Uongozi wake Jimboni hapo, kuwa ni pamoja na Ujenzi wa Madaraja Sita (6) ambayo yataweza kuilinda jamii kutokana na mafuriko ya mvua.


Sheha wa Shehia ya Mtoni Chemchem, Bw. Rashid Jadi Rashid, ameshukuru juhudi za Serikali sambamba na Uongozi wa Jimbo, pamoja na Mamlaka za Mazingira Nchini, kufika hapo kujionea na kuchukua hatua muhimu, katika eneo hilo hatarishi, ambalo hapo kabla likikabiliwa na tishio kubwa la maafa, kutokana na makaazi yaliyokuwepo katikati ya Mtaro usiokuwa salama.


Katika Ziara hiyo, Mheshimiwa Othman, ameambatana na Watendaji na Wataalamu wa Mamlaka ya Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Uongozi wa Wilaya ya Magharibi A Unguja, sambamba na Viongozi wa Jimbo la Mwera.

 

Kitengo cha Habari,

Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,

Alhamis, Septemba 14, 2023.


 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.