Na Fauzia Mussa , Maelezo
Wakala wa Chakula Dawa na vipodozi Zanzibar (ZFDA) imeteketeza jumla ya Tani 130 za mchele mbovu aina ya family gold ulioingizwa Nchini na Kampuni ya Longwide Traders iliyopo maruhubi Wilaya ya Mjini.
Akizungumza wakati wa uteketezaji wa mchele huo huko Jaa kuu Kibele Mkuu wa ukaguzi Bandarini ZFDA Mohamed Shadhil Shauri amesema Mei 13 mwaka huu ZFDA ilizuia kushushwa kwa mchele huo katika Bandari ya Malindi kutokana na kuharibika na kutokufaa kwa matumizi ya binaadamu.
Alisema mchele huo uliharibika kutokana na kujaa Sana katika makontena , hivyo aliwataka wafanyabiashara kuhifadhi bidhaa zao kwa kiasi kinachorushusu hewa kuingia ili kuifanya bidhaa hiyo kuwa salama wakati wote.
Alifahamisha kuwa jukumu la kumlinda mtumiaji ni la watu wote hivyo aliwaomba wafanyabiashara kutoa taarifa kwa wahusika mara Tu wanapoona dalili za kuharibika Kwa bidhaa zao kabla ya kuziingiza sokoni .
Hata hivyo aliwashauri wafanyabiashara kuharakisha taratibu za ushushwaji wa mizigo bandarini ili kuepuka changamoto zinazoweza kujitokeza endapo bidhaa hizo zitakaa kwa muda mrefu ikiwemo kuharibika.
“inawezekana mchele ulipakiwa ukiwa mzima lakini uliharibika kutokana na joto Tu lililomo katika makontena , niwasihi wafanyabiashara mupakie kwa kiasi na kufuata taratibu ili mizigo yenu iweze kutoka kwa wakati ili kuepuka hasara kama hizi.”aliishauri mkuu huyo
Mmiliki wa Bidhaa hiyo Fadhil Muhammad Fadhil alisema mara Tu baada ya kugundua mchele huo umeharibika nakutofaa kwa matumizi ya binaadamu alishirikiana na ZFDA kwa hatua za uteketezaji.
Alisema licha ya kuwa alinunua na kupakia bidhaa hiyo ikiwa salama lakini kuchelewa kufika kwa bidhaa hiyo kulichangia kuharibika,hivyo aliwashauri wafanyabiashara wenzake kuwa makini katika harakati za usafirishaji wa bidhaa ili kukwepa hasara zisizotarajiwa.
"Mchele niliununua ukiwa mzima ila umechelewa kufika ,lile vuke na joto la melini ndio sababu kuu ya bidhaa yangu kuharibika" alisema mmiliki huyo
ZFDA ni TAASISI inayofanyakazi chini ya Sheria Na.2/2006 na marekebisho yake Na.3/2017 yenye jukumu la kudhibiti ubora na usalama wa Bidhaa za chakula kwa kuhakikisha zinakua salama Kwa mtumiaji kabla ya kuingizwa sokoni.
PICHA KWA HISANI YA ZFDA
No comments:
Post a Comment