Na Fauzia Mussa , Maelezo
Wakala wa ,Chakula na Dawa ZFDA Imekamata shehena ya Dawa,vifaa tiba na Vipodozi katika uwanja ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume ulioingizwa Zanzibar kinyume na utaratibu.
Akitoa taarifa kwa Umma, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Dawa na Vipodozi ZFDA Haji Juma Khamis amesema mnamo Septemba 13 mwaka huu wakaguzi wa ZFDA walikamata mzigo huo wenye uzito wa kilo 40 uliongizwa Nchini kutoka Belgium kupitia ndege ya Shirika la Ethopian Airline kwa nambari ya BL (Bill of Loading )071-4959035 bila ya kuwa na kibali .
Alifahamisha kuwa kufuatia uchunguzi uliofanywa na ZFDA Umebaini kuwa vifaa hivyo vilikusudiwa kutolewa msaada katika Vituo vya Afya na Skuli za Wilaya ya Kusini kinyume na utaratibu unaokubalika.
Aidha amesema uchunguzi umebaini uwepo wa dawa zilizomaliza muda wa matumizi takribani miaka kumi,na baadhi ya vifaa tiba vilivyotumika na kufungashwa katika vifungashio visivyo rasmi ndani ya mzigo huo.
Alisema miongoni mwa Dawa zilizopitwa na muda wa matumizi katika mzigo huo ni pamoja na dawa za meno kwaajili ya watoto aina ya ELEMEX, hivyo aliitaka jamii kutokupokea misaada ya Dawa,Vifaa Tiba na Vipodozi ambavyo havikutolewa na Serikali kupitia Wizara ya Afya .
Aidha alifahamisha kuwa bidhaa zote zilizokuwemo katika Shehena hiyo hazikusajiliwa na Wakala wa Chakula na Dawa jambo ambalo ni kinyume na kanuni na Sheria za ZFDA, Hivyo ZFDA imechukua hatua ya kuuzuia mzigo huo usisambae na kufika kwa waliokusudiwa huku taratibu za uteketezaji zikiendelea.
Vilevile aliwataka Wananchi kuendelea kutoa taarifa za uwepo wa bidhaa wanazozitilia mashaka juu ya ubora ,usalama na ufanisi wake ili kumlinda Mtumiaji.
Hata hivyo alitumia fursa hiyo kuwaomba wadau na wahisani kufuata muongozo na taratibu za Wizara ya Afya Zanzibar za kuingiza vifaa kinga na tiba kwa ajili ya misaada ili kuondosha usumbufu unaowezakuijtokeza.
“hata kama Zanzibar ni Maskini lakini huu sio msaada tuanaohitaji ,vitu vimeshatumika vimepitwa na muda ndio mnatuletea,kama muhusika wa shehena hii angelifuata taratibu asingeruhusiwa kuingiza ”Alisema kaimu huyo
No comments:
Post a Comment